Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania ( TPSF), Bwana Godfrey Simbeye ameshauri Vyuo Vikuu kutoa
kipaumbele katika kufundisha ujasiriamali wakati huu ambapo Serikali ya awamu
ya tano imejikita katika kuhakikisha nchi yetu inaingia katika nchi za uchumi
wa kati kwa kuimarisha Uchumi wa Viwanda.
Ameshauri
pia Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini washirikiane kuweka programu za ujasiriamali ili kuwaandaa wahitimu kwa kushirikiana kwa
kuwa hao ndiyo tegemeo katika kuelekea uchumi wa viwanda na hatimae kuingia
uchumi wa kati ifikapo 2025.
Simbeye ameyasema hayo katika kambi
maalum ya Ujasiriamali iliyoandaliwa na Chuo kikuu Mzumbe kwa lengo
la kutoa fursa ya kupeana mbinu na stadi
za ujasiriamali kwa Wanafunzi,Wafanyakazi na Wanajamii wanaokizunguka
Chuo hicho. Simbeye amepongeza Chuo
Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha utaratibu huo na kushauri Vyuo Vikuu vingine nchini kushirikiana na
Chuo Kikuu Mzumbe ili kambi hizi ziweze kushirikisha wanafunzi toka vyuo vyote.
“ Natambua kuwa kambi kama hizi
zinafanyika katika vyuo vingi pia , lakini nishauri tu muungane ili kuongeza
ubora na kufikisha elimu hii kwa wanafunzi wengi zaidi na ninashauri Mzumbe
muwe chachu ya kuanzisha mpango huu.”
Simbeye ameeleza kufurahishwa na kasi ya
serikali ya awamu ya Tano katika kuhamasisha uanzishwaji wa Viwanda na kueleza kuwa wao kama sekta Binafsi
wanaunga mkono juhudi hizo. Simbeye
amesema amefurahishwa kuona ubunifu na uanzishwaji wa viwanda vidogo unaofanywa
na wanafunzi na kuwataka kuhakikisha juhudi zao zinaendelea na viwanda vyao
vinakuwa kufikia viwanda vya kati.
Ameongeza kuwa idadi ya viwanda
nchini bado ni ndogo kwa mujibu wa shirika la Viwango, taarifa ya 2018 inaonesha
kuwa Tanzania ina jumla ya viwanda 53,876 vikiwemo vikubwa ambavyo ni tegemeo
256,viwanda vya kati 173, wakati viwanda vidogo ni 6,957 huku vile vidogo kabisa vikiwa 46, 495, ukilinganisha na nchi jirani
ya Kenya yenye viwanda zaidi 500,000, aliyasema haya akisisitiza kuwa fursa
zipo na lengo ni kuhakikisha viwanda vinakua kufikia viwanda vya kati. Ameeleza
kuwa
TPSF ina jukumu kuu la kuhakikisha inashirikiana na serikali katika
kuhakikisha uendeshaji biashara nchini unakuwa na mazingira rafiki na rahisi na
wezeshi kupitia majadiliano kati ya Sekta Binafsi na Serikali.
Simbeye aliekuwa mzungumzaji mkuu
katika Kambi hii, alishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa Kuwa tayari kufungua milango
ya ushirikiano kwa kutoa ujuzi na uzoefu wa kitaaluma kwa vijana na wananchi wengine wakiwemo waajiriwa na wajasiriamali
ili kuwajengea uwezo. Akitoa shukrani
hizi Simbeye aliahidi kushirikiana na Chuo kikuu Mzumbe kuanzisha Mfuko maalum
utakao saidia kukuza elimu ya Ujasiriamali kwa vijana na kukutanisha vyuo vikuu
na wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kushiriki katika kulea wajasiriamali na
wabunifu wanaoanza.
Awali akizungumza kabla ya
ufunguzi wa kambi hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka alisema wameamua kuanzisha kambi ya
ujasiriamali kwa lengo la kushiriki kwa
vitendo katika azma ya Serikali kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuwaandaa
wahitimu hao ili waweze kuleta tija na kuongeza uzalishaji kupitia Sekta ya
ujasiriamali na viwanda. Prof Kusiluka alisistiza kuwa wakati umefika wa
wahitimu kutumia elimu wanayoipata kujiajiri
zaidi kuliko kutegemea ajira.
Aidha Prof.Kusiluka aliongeza
kuwa uanzishaji wa kambi hiyo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa maendeleo wa Chuo ambao miongoni mwa
mikakati yake ni kuhakikisha Chuo kinahamasisha shughuli za ujasiriamali na
biashara kwa kuanzisha mafunzo maalum kwa Wanachuo na kuwaandaa kujiajiri kwa
kutumia elimu waliyoipata Chuoni hapo. Prof Kusiluka aliongeza kuwa Kambi hizi
zitaendelea kufanyika kila Mwaka na kwa ukubwa zaidi.
Naye Mkuu wa Idara ya Rasilimali
na Ulezi katika shule ya biashara, Dkt Emmanuel Chao alisema maamuzi ya kufanya
kambi hiyo yametokana na kuwepo kwa mitazamo tofauti miongoni mwa Wahitimu wa
Vyuo vikuu nchini kuwa wanapaswa kuajiriwa moja kwa moja pindi wanapomaliza
masomo yao, mtazamo ambao hauendani na hali halisi na hivyo wengi wao kujikuta
wakikosa ajira kutokana na kukosa mbinu za kujiajiri na hivyo Chuo kikuu Mzumbe
kimeona umuhimu wa kuanza kutoa stadi hizo bure kwa wahitimu wote wanaotaka
kujiajiri na kuwasaidia katika kukuza ubunifu na mawazo yao ya kibiashara.
Mgeni rasmi katika kambi hiyo
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ndugu Clifford Tandari, alipongeza hatua ya Chuo Kikuu Mzumbe kkuwa na kambi
hiyo huku akiwataka wanaosimamia pamoja
na chuo kusaidia wajasiriamali na wabunifu walipo katika chuo kuhakikisha
wanasaidiwa kurasimisha biashara zao pamoja na kuzisajili. Tandari amekitaka Chuo Kikuu Mzumbe kusaidia pia kutoa elimu
kwa wajasiamali wengine katika mkoa wa Morogoro ambapo alisema mpaka sasa
unaongoza katika kuwa na viwanda vingi nchini.
Katika kambi hiyo wadau
mbalimbali walipata fursa ya kutoa mafunzo na kutoa uzoefu wao katika biashara
akiwemo Prof Ngowi kutoka , Chuo Kikuu Mzumbe, mjasiriamali mzoefu Kutoka
Kishaga na wengine. Vile vile bidhaa za wabunifu wajasiriamli wanafunzi na
baadhi waliohitimu kutoka Mzumbe zilizinduliwa.
Makamu
Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, akifurahi pamoja na Wanafunzi
Wajasiriamali walioshiriki kambi ya Ujasiriamali na kuzindua bidhaa zao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, akizindua bidhaa ya mvinyo iliyotengenezwa na wafanyakazi wajasiriamali wa Chuo Kikuu Mzumbe, mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, wakati wa Kambi ya Ujasiriamali iliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu na stadi za ujasiriamali wanafunzi, wafanyakazi na jamii inayokizunguka chuo hicho.
Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka, akizindua moja ya
bidhaa za Wananchuo walioshiriki kambi ya Ujasiriamali.
Mjasiriamali akinadi bidhaa zake kwa Washiriki.
Baaadhi ya washiriki wa kambi ya ujasiriamali wakiangalia bidhaa zilizoletwa katika kambi hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro (mwenyesuti nyeusi) akiendelea kupokea
maelezo kuhusu bidhaa kwa wajasiriamali walioshiriki kambi hiyo. Kushoto
kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka.
Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda, akijadiliana
jambo na Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe (mwenye shati
jeupe) mbele ya mgeni rasmi,mwenyekiti wa TPSF na Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Mzumbe
Mjasiriamali akitoa maelezo ya bidhaa zake kwa Mgeni Rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro ndg.Cliford Tandari (katikati), kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sekta Binafsi Tanzania TPSF na kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda, akimpongeza Mwanafunzi wa Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe Talib Mlilima aliyejikita katika ujasiriamali wa kubuni na kushona suti baada ya kuzindua bidhaa yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Clifor Tandari akifurahi pamoja na Wanafunzi wakati akizindua bidhaa za Wanachuo hao.Anayeshuhudia pembeni ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro akipata maelezo kutoka kwa Mjasiriamali (hayupo pichani)
Mjasiriamali akitoa maelezo ya bidhaa zake kwa Mgeni Rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro ndg.Cliford Tandari (katikati), kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sekta Binafsi Tanzania TPSF na kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda, akimpongeza Mwanafunzi wa Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe Talib Mlilima aliyejikita katika ujasiriamali wa kubuni na kushona suti baada ya kuzindua bidhaa yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Clifor Tandari akifurahi pamoja na Wanafunzi wakati akizindua bidhaa za Wanachuo hao.Anayeshuhudia pembeni ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro akipata maelezo kutoka kwa Mjasiriamali (hayupo pichani)
No comments:
Post a Comment