HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2018

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WAASWA KUWA WAADILIFU KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Bw. Eric Shitindi akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo (hawapo pichani) juu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Peter Kalonga. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU – KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU)
 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Peter Kalonga, akizungumza na Watumishi wa Ofisi wakati wa Mkutano wa wafanyakazi wa Ofisi hiyo walipokutana ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 22, 2018 Jijini Dodoma.
 Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo (Hayupo pichani) walipokutana katika kuiadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma.
  NA MWANDISHI WETU
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu wameaswa kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ili kuwa na utendaji unaofuata sheria, kanuni na Maadili ya Utumishi wa umma.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu)Bw.Eric Shitindi alipokutana na wafanyakazi wa ofisi yake Dodoma kwa lengo la kuiadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka kuanzia Juni 16-23 Barani Afrika ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni;

“mapambano dhidi ya rushwa kwa kushirikiana na wadau na kujenga uongozi bora ili kufikia malengo ya ajenda 2063 ya umoja wa afrika na malengo ya maendeleo endelevu”

Katika kuiadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ipo kisheria Katibu Mkuu huyo aliwataka Watumishi wa ofisi yake kuendelea kuwajibika huku wakikwepa mianya yote ya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa haki na usawa.

“Yapo maeneo mengi yenye viashiria vya rushwa, hivyo ni vyema watumishi wakafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili waweze kuwa na bidii katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kuepukana na mazingira ya ushawishi wa kupokea rushwa”, alieleza Shitindi.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa ofisi hiyo, Bw. Peter Kalongo aliunga mkono kwa kuwataka watumishi wote kuifanyia kazi rai hiyo kwa vitendo na kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayolenga kuendelea na mapambano dhidi ya rushwa ili kujenga uongozi bora.

 “Ni vyema sasa watumishi wote kuendelea kuepuka mazingira yote ya rushwa katika utendaji wetu, tutahakikisha mapambano haya yanaendelea kwa Kushirikiana na TAKUKURU na wadau mbalimbali ili kuwaelimisha watumishi juu ya njia za kupambana na rushwa”, alisisitiza Kalonga.

Kwa Upande wake Kaimu Mkuu Kitengo cha Wenye Ulemavu Bw. Jacob Mwinula amesema kuwa watumishi wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia haki na usawa kuepuka mazingira ya rushwa ili kulihudumia kundi la wenye ulemavu kwa kuzingati sheria zilizopo.

“Kufahamu kanuni na sheria kutaweza kuwasidia watumishi kufanya kazi na watafata misingi ya utumishi wa umma na kwenye mazingira salama, yenye ushirikiano kutokana na dhamana waliyopewa kusaidia watu wenye ulemavu kupata haki na huduma zao”, alisema Mwinula

No comments:

Post a Comment

Pages