*Aagiza
viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wabadilike
*Ataka
wasimamie wananchi waachane na matumizi ya mkaa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote
za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa
matumizi ya kuni na mkaa.
“Wizara, taasisi na mashirika yote ya Serikali na binafsi
pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili
ya kupikia au shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati mbadala ili
matumizi ya mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na
mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa
maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati
Mbadala.”
Waziri Mkuu amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo
ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha
wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake
watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu
na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Ili kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali
vya ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze
kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia
ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na
majengo makubwa.
“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha
kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji
waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane
na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani
500,000 za mkaa kwa mwaka.
“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa
wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi
gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya,
za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni
lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”
“Meya ametoa fursa na amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni.
Tengenezeni bajeti kupitia Mabaraza ya Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali
wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa teknolojia hii kwenye maeneo yenu.
Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe watengeneze mashine nyingi
zaidi na zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze kutumia teknonolojia hiyo
kupikia,” alisisitiza.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es
Salaam wafuatilie kwa karibu usambazaji wa teknolojia hiyo.
Kwa upande
wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali ya mazingira hapa nchini ni
mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu waishio mijini.
“Hali ya mazingira nchini mwetu ni mbaya sana na inawezekana watu
wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa sababu mahitaji yao yote
wanayapata sokoni na madukani,” alisema.
“Wenzetu wa mikoani na vijijii wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba
wanataabika kwa sababu kipato chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa
mazingira,” alisema.
Alisema mazingira yanafungamana na utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji
na kwamba maendeleo ya nchi pia yamefungamana moja kwa moja na mazingira.
“Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya
mkaa wote unaozalishwa nchini Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,”
alisema.
Waziri Makamba alisema taasisi za Serikali kama vyuo, magereza, hospitali
na shule zinaongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu
mkubwa wa mazingira.
Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao
30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu kila siku.
“Chuo hiki kina migahawa tisa, kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna
mgahawa mmoja mdogo unatumia magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa
unatumia magunia mangapi?” alihoji.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu
ambayo ni siku ya kilele. Pia wiki nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na
mjadala wa kitaifa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
ALHAMISI, MEI 31,
2018.
No comments:
Post a Comment