Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeliteua Gereza la Kwitanga
lililopo wilayani Kigoma kuwa kituo kikuu cha uzalishaji wa zao la
michikichi nchini.
Hivyo
ameuagiza uongozi wa gereza hilo waongeze nguvu katika uzalishaji wa
michikichi kwa kupanua mashamba na kuongeza askari wenye ujuzi wa kilimo
cha michikichi na kupanda miche mipya ya michikichi na kukata ya
zamani.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 29, 2018) wakati alipotembelea
gereza hilo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi yenye
lengo la kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma.
Amesema
Serikali imedhamiria kwa dhati kufufua kilimo cha zao la michikichi
mkoani Kigoma, hivyo kila mwananchi lazima awe na shamba la michikichi.
Katia hatua nyingine,
Waziri Mkuu ameuagiza Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma Bw. Sabas Matolo
kuhakikisha Gereza la Kwitanga linawezeshwa kwa kuwa na zana bora na za
kisasa za kilimo yakiwemo matrekta na vifaa vya kuvunia ili waweze
kuongeza uzalishaji wa mafuta.
Pia,
Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Matolo awahamishe askari ambao ni wataalamu
wa kilimo wenye ujuzi wa zao la michikichi kutoka kwenye Magereza
mengine mkoani Kigoma na kuwahamishia katika gereza la Kwitanga ili
kuimarisha uzalishaji.
Awali,
Mkuu wa gereza hilo Bw. Majuto Masila alisema ili kilimo cha michikichi
na uzalishaji wa mafuta uweze kuwa na tija, wanahitaji wafungwa
wasiopungua 300 wawepo kila siku gerezani hapo ili kumudu shughuli za
shamba hilo. Kwa sasa kuna wafungwa 112.
"Uzalishaji
wa mafuta kwa miaka mitatu mfululizo gerezani Kwitanga ni kama
ifuatavyo mwaka 2015/2016 tulizalisha lita 16,094, mwaka 2016/2017 lita
12,674, na mwaka 2017/2018 tulizalisha lita 16,000," alisema.
Alisema
mafuta yanayozalishwa gerezani hapo yanatumika katika kulisha wafungwa
wa gereza hilo la Kwitanga, Bangwe, Kasulu, na Kibondo. Ziada ya mafuta
hutumika kulisha wafungwa magereza ya mikoa ya Kagera, Mwanza,
Shinyanga, Singida, Dodoma, Morogoro na Tabora.
Baada
ya kutoka katika Gereza la Kwitanga, Waziri Mkuu alitembea shamba
darasa na eneo la kuzalisha miche ya michikichi la Seed Change katika
eneo la Mungonya na kuziagiza halmashauri zote zinazolima michikichi
mkoani Kigoma kwenda kununua mbegu kwenye shamba hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 29, 2018.
No comments:
Post a Comment