HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 29, 2018

WABUNGE WA KIGOMA WARIDHISHWA NA UTENDAJI WA SERIKALI

*Waipongeza kwa kampeni ya kuhamasisha kilimo cha michikichi

WABUNGE wa mkoa wa Kigoma wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi kwa sababu litasaidia kuondoa umasiki kwa wananchi wa mkoa huo.

Wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba Serikali kulifufua zao hilo kwa kuwa ndilo zao kubwa la biashara linalotegemewa na wananchi wengi wa mkoa huo, hivyo kitendo cha kuanzisha kampeni hiyo kinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kuwakwamua wananchi.

Wakizungumza kwa jana (Jumamosi, Julai 28, 2018) wabunge hao waliahidi kushirikiana na Serikali bega kwa bega kuhakikisha kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi linafanikiwa kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Wabunge hao waliyasema hayo  baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kuhamasisha kilimo cha zao la michikichi katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma. Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau wa zao hilo.

Miongoni mwa wabunge hao ni mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye aliipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrfu cha wananchi wa mkoa huo cha kufufuliwa kwa zao la michikichi kwa kuwa litakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Kigoma.

“Nakupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa kitendo hiki cha kufufua zao la michikichi kwani hiki ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigoma kwa hatu hii naamini kuwa leo hata waliotangulia mbele ya haki watakuwa wanatabasamu huko waliko,”.

Pia mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi na viongozi wa mkoa wa Kigoma kuwa ni vema wakashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha zao hilo linafufuliwa kwa watu kuchangamkia fursa ya kupanda michikichi kwenye mashamba yao.

Mbunge mwingine wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba alisema changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa mkoa huo ni upatikanaji wa mbegu bora za michikichi, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia katika upatikanaji wa mbegu.


Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Trade Mark East Africa, Bw. John Ulanga alisema walifanya utafiti kuhusu zao la michikichi na walibaini kuwa kuna soko kubwa la mafuta ya mawese ndani ya nchi yetu, pamoja na nchi za jirani ila uzalishaji wa mafuta hayo ndani ya nchi bado ni mdogo sana.

No comments:

Post a Comment

Pages