*Ataka ushirika wa sasa urejeshe matumaini ya
wakulima
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi
wapya wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga wajipime kama wako tayari
kuwatumikia wananchi na kama sivyo waachie ngazi.
Ametoa onyo hilo jana (Ijumaa,
Julai 13, 2018) wakati akizungumza na
mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani mara baada ya
kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya
ziara yake ya siku tano mkoani humo, aliwataka wajumbe hao wajitafakari upya na
kujihoji kama wameomba vyeo hivyo kwa ajili ya kupata utajiri ama kuwatumikia
wananchi.
“Napenda kusisitiza kwamba ule mfumo wa zamani
wa ushirika hivi sasa haupo. Kama uliomba cheo hicho kwa ajili ya kupata
utajiri, ni bora ujiondoe sasa hivi, njoo uniambie wakati bado niko kwenye
ziara ya mkoa huu, tutatafuta wajumbe wengine ambao ni waaminifu,” alisema.
“Nasisitiza kwa viongozi wa AMCOS na wa
SHIRECU, mmeomba vyeo hivyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na siyo
kujinufaisha binafsi,” alisisitiza.
Alisema tofauti na ilivyokuwa awali, Serikali
ya awamu ya tano inataka kuona ushirika wa sasa ukirejesha matumaini kwa
wananchi.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zamani,
ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio lakini kutokana na hali
ilivyobadilika, jambo hilo lilikuwa haliwezekani. “Tunataka ushirika wa sasa
ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba
bora,” alisema.
Wakati huohuo, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bw. Elias Kwandikwa alisema barabara
ya kutoka Kolandoto hadi Igelekelo imeshafanyiwa usanifu na kwamba Serikali ya
Ujerumani imeanza mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuhusu ujenzi wake.
Alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara
alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Mwangongo waliokuwa
wakisubiri kumsikiliza Waziri Mkuu.
“Kazi ya usanifu wa barabara hiyo imekamilika,
tumeanza mazungumzo ya kutafuta wafadhili. Ujenzi wake ukikamilika, utakuwa
umerahisisha kuunganisha mkoa huu na mikoa ya Singida, Arusha na Manyara.”
“Kutoka Shinyanga hadi Singida tutakuwa
tumepunguza km. 250, wakati kutoka Shinyanga jadi Karatu tutakuwa tumepunguza
km. 400 badala ya kupita kwanza Nzega, uende Singida hadi Karatu,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani
Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 14, 2018.
No comments:
Post a Comment