*Asisitiza wananchi wajiunge na Bima ya Afya
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanaume
wote wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakapime afya zao ili kubaini kama
wameambukizwa virusi vya UKIMWI au la.
Ametoa rai hiyo jana (Ijumaa, Julai
13, 2018) wakati akizungumza na mamia
ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa
hadhara mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani
Kishapu mkoani Shinyanga.
“Napenda kusisitiza kwa akinababa wote kwamba ukimwi
bado upo na wanaume hamuendi kupima, ni wagumu kwenda kupima eti kwa sababu
mnawategemea wake zenu waende kupima.”
“Unamwambia mama aende kupima virusi vya UKIMWI
akija na majibu ukajua hana maambukizi, wewe huku unashangilia kwamba uko
salama. Hapana, nendeni mkapime kwa sababu kila mmoja na vyanzo vyake vya
kupata maambukizi,” alisisitiza.
Alisema maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) katika
wilaya ya Kishapu yako kwenye asimilia 2.1 ikilinganishwa na kiwango cha
maambukizi ya VVU kwa mkoa mzima ambayo kwa sasa ni asilimia tano.
“Ni vema familia zikapima VVU ili mjue hali zenu na
muishi kwa furaha na kama kuna mmoja ameambukizwa basi aanze tiba mara moja,”
alisema Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku
tano mkoani humo.
Alisema
katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Tanzania inatekeleza malengo ya 90-90-90
ifikapo mwaka 2020. Lengo ni kuhakikisha
kuwa asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia
90 ya waliopima VVU na kugundulika kuwa wana maambukizo wapatiwe dawa za
kufubaza VVU (ARVs); na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza
VVU.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka wakazi wa wilaya ya Kishapu wajiunge na bima ya afya ili waweze kupata tiba hata wakati hawana fedha.
“Halmashauri yenu imeweka kiwango cha sh. 30,000 kwa
mwaka ambapo baba, mama na watoto wanne watakaojiunga na huduma hii ya afya ya
jamii, watapata matibabu bure kwa muda wa mwaka mzima mahali popote.”
“Ninawaomba mjiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)
ambao utakuwezesha kupata tiba siku ambayo huna hela mfukoni au nyumbani. Pia
utakuwa na uhakika wa kupata matibabu bure kwenye zahanati au kituo cha afya
chochote kile katika katika wilaya hii,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani
Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 14, 2018.
No comments:
Post a Comment