HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 28, 2018

AfDB YATEKELEZA MIRADI YA SH. TRLIONI 4.4 NCHINI TANZANIA

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wa pili kulia, akiagana na mgeni wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeiwakilisha Marekani Bw. J. Steven Dowd (wa pili kushoto) Nje ya jengo la Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa AfDB Dkt. Alex Mubiru na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayeshughulikia nchi nane za Afrika Dkt. Nyamajeje Weggoro. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).
Mkurugenzi Mtendaji wa  wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeiwakilisha Marekani Bw. J. Steven Dowd akieleza nia yake ya kuzungumza na Bodi ya Benki hiyo ili kuangalia namna ya kusaidia kutekeleza miradi ya kipaumbele nchini Tanzania ikiwemo ya Umeme na Reli alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari (Hawapo Pichani) Jijini Dar es Salaam.


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinapewa fedha nyingi  kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika Sekta ya Nishati, Maji, Kilimo na Barabara ili kuchochea uchumi na kutimiza malengo ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo  mwaka 2025 ambapo mpaka sasa Benki hiyo imewekeza nchini zaidi ya  shilingi trilioni 4.4.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na  Mkurugenzi wa  wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeiwakilisha Marekani Bw. J. Steven Dowd katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, alieleza kuwa Tanzania inapata fedha nyingi za kutekeleza miradi kutoka Benki ya AfDB kutokana na vipaumbele vya Benki hiyo kuendana na vipaumbele vya Serikali ya Tanzania katika Awamu ya Tano ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
“Miradi inayotekelezwa kwa fedha za AfDB ni pamoja na mradi wa kusafirisha umeme kutoka Mbeya, Sumbawanga hadi Nyakanazi utakao gharimu shilingi dola za Marekani milioni 123, miradi mingine ni ile ya ushirikiano na Sekta Binafsi (Dola Milioni 57.6m), ujenzi wa barabara ya Nyakanazi mpaka Burundi kupitia Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma na pia mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato Jijini Dodoma ambao AfDB imeahidi kutoa shilingi bilioni 200 kwa kuanzia”, alieleza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa  wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeiwakilisha Marekani Bw. J. Steven Dowd, alisema kuwa ameona dhamira ya dhati ya Tanzania katika kufikia malengo tarajiwa hivyo anaangalia uwezekano wa kukaa na bodi ya Benki ya AfDB ili kuendelea kuisaidia Tanzania katika miradi mikubwa ya Nishati ya Umeme na Ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Pia ameahidi kuwashawishi wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna mazingira mazuri ya uwekezaji na kuishauri Serikali kuweka mazingira mazuri zaidi ya kimikataba kati yake na wawekezaji ili waweze kuwa na uhakikak wa usalama wa uwekezaji wao.
Aliahidi kutumia ushawishi wake katika masuala ya biashara na uwekezaji ili wafanyabiashara wengi kutoka nchji hiyo waweze kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini na kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kukuza uchumi wan chi na watu wake.
Alisema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ni mtu wa vitendo kuliko maneno na kuihakikishia Tanzania kwamba itapata ushirikiano mkubwa kutoka Serikali ya nchi hiyo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais FDkt. John Pombe Magufuli za kujenga uchumi wan chi.
Akieleza kuhusu maombi ya Serikali ya kutaka Benki yake isaidie ujenzi wa MIradi mikubwa ya Maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya kiwango cha Kimataifa-SGR, Mradi mkubwa wa kufua umeme kutoka Mto Rufiji, na miundombinu mbalimbali, Bw. J. Steven Dowd alisema kuwa wataijadili miradi hiyo ili kuangalia namna ya kuifadhili.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango na mgeni wake kumalizika, Mkurugenzi wa AfDB Kanda ya Afrika, Dkt. Nyamajeje Weggoro, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki yenye hisa nyingi katika Benki hiyo hivyo kunufaika katika fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
“Tanzania  inahisa takribani asilimia moja kati ya asilimia tano zinazomilikiwa na nchi nane ikiwemo Uganda, Rwanda, Ethiopia, Kenya na Sudani Kusini na pia inatekeleza miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika yenye thamani ya Sh.Trilioni 4.4”, a;lieleza Dkt. Weggoro.
Waziri Mpango amemshukuru Bw. Dowd kwa kuitembelea Tanzania na kuonesha dhamira ya kusaidia miradi ya maendeleo na akaahidi kuendeleza ushirikiano na Benki ya AfDB na pia Marekani.

No comments:

Post a Comment

Pages