HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 28, 2018

DKT. MPANGO: AAGIZA MAKONTENA YA MAKONDA YAPIGWE MNADA LICHA YA VITISHO VYAKE

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwasili kukagua Kontena  ishirini za Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul makonda, zilizo na Samani vikiwemo viti na Meza katika Bandari ya Dar es Salaam.
Afisa Forodha Mfawidhi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bandari ya Dar es Salaam Bw. Stephano Mathias, akitoa maelezo  kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) kuhusu bidhaa za samani za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, zinazodaiwa kodi ya Sh. Bilioni 1.2, huku mmiliki wake akijulikana kwa jina la Paul Makonda.
Kamishna wa Forodha  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Benny Usaje (katikati) akieleza kuwa amepokea maagizo ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) mwenye dhamana ya kodi nchini kuhakikisha kodi ya kiasi cha Sh. Bilioni 1.2 inalipwa kwa mujibu wa sheria kwenye Kontena hizo 20 za RC Paul Makonda.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akitoa maagizo kwa Kamishna wa Forodha  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Benny Usaje, ya kuendelea kupigwa mnada kwa Kontena ishirini za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, zinazodaiwa kodi ya Sh. Bilioni 1.2 ili Serikali iweze kupata kodi yake kama kodi kutoka kwa mmiliki wa Kontena hizo hatalipa kodi kwa wakati.
Baadhi ya viti vilivyopo katika Kontena zinazodaiwa kodi ya Sh. Bilioni 1.2, wakati Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alipofika kukagua na kujiridhisha kama kuna taratibu za kodi zimekiukwa ili mzigo huo wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda uweze kuendelea kupigwa mnada.


 Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika eneo la kuhifadhia makontena-Bandari Kavu Dar es Salaam (DICD), na kukagua makontena 20 yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA kuendelea na mnada wa makontena hayo ili kupata kodi ya Serikali inayokadiriwa kufikia shilingi bilioni 1.2.
Dkt. Mpango amesema kuwa kodi hiyo inadaiwa kwa mujibu wa sheria za nchi baada ya mwenye mali kushindwa kulipa kodi na kwamba amesikitishwa na vitisho vinavyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa na vilivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini  akitumia vifungu vya Biblia kwamba yeyote atakaye nunua mzigo huo atalaaniwa.
"Sheria za nchi hazichagua sura wala cheo cha mtu, na mimi ndicho nilicho apa, kutekeleza sheria za nchi, sheria za kodi, ndiyo dhamana niliyo pewa kwahiyo Kamishna, simamia sheria za kodi bila kuyumba" alisisitiza Dkt. Mpango akitoa maelekezo kwa Kamisha wa Forodha Bw. Ben Usaje.
Alifafanua kuwa mzigo wa Samani ulioagizwa kutoka nje ya nchi hauna msamaha wa kodi na kwamba huyo aliye agiza (RC Paul Makonda) alipe kodi stahidi na asipo lipa kodi hiyo mchakato unaoendelea wa kuyapiga mnada makontena hayo uendelee.
"Napenda niwaombe viongozi wenzangu Serikalini, ni muhimu tukachuja maneno! unasema mtu anayekuja kununua samani atapata laana, tena laana ya Mungu, kwa nini tunamhusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii" alieleza kwa masikitiko Dkt. Mpango
Dkt. Mpango alitoa wito kwa watanzania wanaotaka kununua bidhaa hizo ambazo nyingi ni vifaa vinavyoweza kutumika shuleni ama maofisini kama vile viti meza na makabati, kujitokeza bila hofu kununua mali hizo.
 Aliwaomba walimu na wanafunzi wasiwe na wasiwasi na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua na kuwekeza kwenye elimu kwa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwezi kulipa ada ya wanafunzi ili wasome bila kulipa ada na ina mpango madhubuti wa kuboresha miundombinu ya elimu nchi nzima ikiwemo ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu.
"Tunawapenda na kuwathamini sana walimu wetu, asitokee mtu yeyote  akaanza kuwaambia hadithi kama vile Serikali hii inawapuuza! si kweli hata kidogo" Aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake, Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Ben Usaje, alimweleza Dkt. Philip Mpango kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, aliwasilisha maombi ya kutaka kupewa msamaha wa kodi wa makontena 36 yenye samani kutoka Diapora nchini Marekani.
Alisema kuwa kati ya makontena hayo, yaliyoingia nchini ni makontena 20 ambayo yanadaiwa kodi ya shilingi bilioni 1.2 na kwamba utaratibu kwa kumtaka Paul Makonda alipe kodi hiyo ili aruhusiwe kuyachukua makontena hayo ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba mpaka sasa hajayachukua ndio maana yanapigwa mnada.
Naye aliwatahadharisha watu wanao tumia masuala ya siasa na uongozi Serikalini kutaka kukwepa kulipa kodi a kwamba suala la kodi za samani zinaonekana ziko juu kwa sababu Bunge lilitunga sheria hiyo ili kulinda soko la ndani la samani na kuweka sheria ya kutokuwepo kwa msamaha wowote wa kodi kwenye bidhaa kama hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages