Mlango wa kuingilia abiria kwenye
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wanaotoka nje ya
nchi ambao baadhi ya ndege zimelengwa kutokana na abiria wake aidha kupita au
kuanzia safari kwenye nchi ya Kongo
iliyotangazwa kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola
Eneo maalum la ukaguzi wa afya kwa
abiria mara baada ya kuingia kwenye sehemu ya wanaowasili kutoka nje ya nchi,
ambapo kumefungwa mashine maalum zenye kuonesha joto la mwili na likizidi 38
abiria huyo hufanyiwa mahojiano ya afya yake, kwa kuwa moja ya dalili za
ugonjwa wa Ebola ni kuwa na joto kali.
Mmoja wa abiria aliyewasili na ndege
ya Rwanda Air kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),
akinawa mikono kwa dawa maalum inayoua vijidudu vya maradhi mbalimbali
yanayoambukiza, ukiwemo Ebola uliotangazwa hivi karibuni umeibuka nchini Kongo.
Afisa Afya Mfawidhi wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dkt. George Ndaki akionesha
mashine maalum inayompima abiria (thermo scanners) mara anapopita eneo la
ukaguzi wa afya, ambapo linakuwa likisomwa na Afisa Afya kwenye komputa iliyopo
(kulia). JNIA wamejidhatiti na makonjwa ya milipuko ukiwemo wa ebola
uliotangazwa kuwepo nchini Kongo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kulia), akizungumza
na waandishi wa habari juu ya udhibiti wa magonjwa ya mlipuko kwenye kiwanja
hicho. Hivi karibuni ugonjwa wa Ebola umetangazwa kutokea nchini Kongo.
Bango linalotoa maelezo yanayohusiana
na ugonjwa hatari wa Ebola likiwa eneo la wasafiri wanaowasili kutoka nje ya
nchi kweney Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Na Mwandishi Wetu
KITENGO cha Afya katika Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kimeweka udhibiti madhubuti
wa kujikinga na usambazaji wa magonjwa ambukizi ukiwemo ugonjwa wa Ebola.
Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi
vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni,
puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka.
Hivi karibuni umetangazwa kutokea nchini
Kongo na kusababisha vifo.
Akizungumzia kuhusiana na mikakati hiyo
ya kupambana na magonjwa ambukizi ukiwemo wa Ebola, Afisa Afya Mfawidhi
wa JNIA, Dk. George Ndaki amesema wanatoa mafunzo kwa watumishi na wahusika
wote wanaotumia kiwanja hicho katika kujikinga na magonjwa hayo.
“Sisi tumejiandaa vizuri na
tumeshafanya jitihada zote tumeshatoa maelekezo, mafunzo na kamati mbalimbali
za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza, ikiwemo sisi
wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote wanaotoka katika nchi hatarishi”,
amesema Dkt. Ndaki.
Aidha akizungumzia kuhusiana na
utaratibu ambao Kiwanja kimeweka ili kuhakikisha abiria wenye maambukizi
wanapokelewa kwa tahadhari, ambapo wanapowasili na ndege zinazotoka nje ya nchi
zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi zinazoshirikiana na Kongo
hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalum mara waingiapo katika eneo la
kuwasili.
Pia abiria hao wanapoingia katika lango
la kuwasili la abiria kutoka nje ya nchi, kumekuwa na mashine maalum inaangalia
joto la mwili na likizidi nyuzi joto 38 wanamtaka kutoa maelezo Zaidi ya afya
yake.
“Abiria wote wanapowasili hupita katika
eneo maalum ambalo wote hutakiwa kuosha mikono, lakini pia kuna mashine ambazo
zimewekwa ili kuweza kuwatambua abiria ambao wanawasili wakiwa na hali ya joto
isiyokuwa ya kawaida mfano kuwa na joto la juu sana kuanzia 38oC,
ukiachana na hilo kuna fomu maalum ambazo abiria wanapowasili hujaza na pia
taarifa kutoka kwa rubani wa ndege kama kuna abiria ana maambukizi kwenye
ndege. Baada ya kumtambua mgonjwa basi atapitishwa katika njia ya tofauti na
abiria wengine na kupakiwa katika gari la wagonjwa na kupelekwa Temeke
Hospital,” amesema Dk. Ndaki.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi juu
taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola, ameeleza kuwa tayari JNIA wanazo taarifa
za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua
abiria wanaotoka nje ya nchi.
“Kwanza kabisa kwa abiria wote ambao
wanatokea katika nchi ambazo zinasadikika kuwa na maambukizi wanapowasili
wanakuwa sanitized (wanaosha mikono na dawa maalum) ili wasiweze kuleta
maambukizi ndani, lakini pia tuna thermo scanners (mashine ambazo
zinaangalia hali ya joto la mtu) anapowasili ambapo tunapogundua mgonjwa
anamatatizo tunapeleka isolation (Chumba cha wagonjwa wa kipekee) na baada ya
hapo anapelekwa katika vyumba vya waonjwa waliotengwa katika hospitali ya
Temeke” alibainisha Bw. Rwegasha.
Katika hatua nyingine Dk. Ndaki amesema
mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ambaye amebainika kuwa na ugonjwa wa Ebola
kupitia JNIA.
Dk Ndaki ametaja namna ya kujikinga na
ugonjwa wa Ebola ni pamoja na kuepuka kugusa damu, machozi, jasho, matapishi,
kamasi, mkojo au kinyesi cha mtu mwenye dalili za ugonjwa; pia mtu hatakiwi
kugusa, kuosha au kuzika maiti ya aliyekufa kwa Ebola; pia usiguse au kula
wanyama kama popo, sokwe au swala wa msituni.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali,
maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele ma
kutokwa damu
“Natoa wito tu kwa wananchi kuhakikisha
wanafuata taratibu zote tulizoziweka ili kuhakikisha kwamba hatupati mgonjwa
yeyote katika nchi yetu. Kama kila mtu atatekeleza wajibu wake kwa abiria kufuata
taratibu, wanaosimamia masuala ya afya wakitimiza wajibu wao, na Kiwanja
kikitimiza wajibu wake basi hakika magonjwa ya mlipuko hayataweza kufika katika
nchi yetu” alieleza Dkt. Ndaki.
No comments:
Post a Comment