*Akerwa na maamuzi kufanyika bila Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu kuarifiwa
*Asema Wizara yake imeamua kubadili taswira ya Ofisi
yake
WAZIRI
wa Katiba na Sheria, Prof.
Palamagamba Kabudi amesema kuanzia sasa mawakili walioko kwenye Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa
na taasisi za Serikali watakuwa ni Mawakili wa Serikali.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) kabla hajamkaribisha Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ahutubie wageni waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi
ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
“Kwa miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio
kwenye utumishi wa umma. Maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” alisema.
Alisema hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa
ikiisababishia Serikali kuingia kwenye migogoro na kuingia hasara. “Baada ya
mabadiliko haya, wanasheria wote walioajiriwa katika utumishi wa umma wanakuwa
wanafanya kazi na kutumia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya wizara
zao, taasisi zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.
“Vilevile wanasheria hao watakuwa chini ya uangalizi wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali. Nia ya mabadiliko haya ni kumuwezesha Mwanasheria Mkuu wa
Serikali awe na usimamizi juu yao na kuwazuia kufanya kazi bila kufuata maelekezo
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
Prof. Kabudi alisema mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, TANESCO
nayo pia yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuepuka
kuitia Serikali hasara. “Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mashirika haya,
lakini kuna maamuzi yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haina taarifa,”
amesema.
“Kutokana na marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali itaratibu na kusimamia Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi hiyo
na wanasheria wote katika Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za
Serikali ambao sasa watakuwa ni Mawakili wa Serikali. Aidha, Mawakili wa
Serikali walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na
Wakili Mkuu wa Serikali,” amesema.
Amesema marekebisho hayo yanatokana
na marekebisho ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia matangazo
ya Serikali Na. 48, 49 na 50 ya tarehe 13 Februari, 2018.
“Leo tunamshukuru sana Mheshimiwa
Rais kwa kufanya marekebisho hayo. Rais alianzisha Ofisi huru ya Taifa ya
Mashtaka kuchukua nafasi ya iliyokuwa Divisheni ya Mashtaka chini ya Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vilevile, Rais alianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendeshaji wa
mashauri ya madai yakiwemo ya kikatiba ambayo Serikali ni mdaawa ambayo awali
yalikuwa yakishughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.
Amesema marekebisho hayo
yanakusudia kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai nchini
hususani utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutenganisha shughuli za upelelezi
na uendeshaji wa mashtaka. “Kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
kunalenga kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai na pia
kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarika katika weledi na
ubobezi wa kitaalamu katika kuishauri Serikali na kuandika Miswada ya Sheria
kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika tasnia ya sheria kitaifa, kikanda na
kimataifa,” ameongeza.
Hata hivyo, Prof. Kabudi alionya kwamba mabadiliko yoyote
hayawezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa kama watendaji hawatabadili mtizamo wao. Ni
kweli muundo uliobadilishwa ulikaa kwa miaka mingi na inawezekana mambo mengi
yalikuwa yanafanyika kwa mazoea. “Kutokana na mabadiliko haya, tunakiri kuwa mitizamo yetu na ya watumishi wenzetu lazima
ibadilike. Tumejipanga kuhakikisha kuwa watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea ili
wasiwe na tashwishwi wala ajizi katika kutekeleza majukumu ya umma.”
“In public service, learn to swallow your
pride. In public service, learn to learn your limits. In public service, learn
to obey the authority above you, and if you don’t, resign and quit,” alisisitiza.
“Tumejipanga
kufanya kazi kwa weledi na katika hili tutaweka mikakati ya kuwaongezea
watumishi wa ofisi hizi ujuzi katika maeneo mahususi, na katika hilo tutaweka
mipango ya kuwafanyia placement ndani
na nje ya nchi ili wapate ujuzi mahususi na kuhakikisha wanapata mafunzo ya
muda mfupi na mrefu katika maeneo mbalimbali.
Alisema wameanza mkakati wa
kuanzisha umoja wa wanasheria walio katika utumishi wa umma ili kuwawezesha
kukutana mara kwa mara na kwamba Agosti 30-31 mwaka huu, wanatarajia kufanya mkutano
huo ili kuwaunganisha wanasheria wote wajione wanafanya kazi moja na katika
Serikali moja.
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa
Serikiali, Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka jijini
Dodoma Agosti 15, 2018. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji
la Dodoma, Godwin Kunambi, Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Devis
Mwamfupe, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde, Waziri wa
Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, Mkuu wa wilaya ya Dodoma,
Patrobas Katambi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria , Profesa Sifuni Mchome,
Mkurugenzi wa Mshtaka, Biswalo Mganga na kulia ni Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali, Dkt. Ally Posi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama vitabu wakati alipotembelea
maktaba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa
Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka aliyoizindua jijini Dodoma,
Agosti 15, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkuu wa wilaya ya Dodoma,
Patrobas Katambi baada ya kuzindua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mshtaka jijini
Dodoma, Agosti 15, 2018. Kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria,
Profesa, Paramagamba Kabudi na kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Seriakli,
Dkt. Adelardus Kilangi.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na
viongozi walioshirki katika uzinduzi wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka jijini
Dodoma, Agosti 15, 2018. Waliokaa wanne kushoto ni Waziri wa Katiba na
Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi na watatu kushoto ni Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Watatu kulia ni Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi na wanne kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Dodoma, Patrobas Katambi. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment