WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa kuibuka kwa sekta za mafuta na gesi hapa nchini kumeleta haja
ya kuwa na wabobezi wa masuala hayo katika taaluma ya sheria.
“Taaluma ya
sheria kwa sasa inahitaji kuwepo kwa ubobezi. Imekuwa si rahisi tena kwa
mwanasheria kuwa na utaalamu wa kutosha katika maeneo yote ya sheria. Hii
inatokana na ukweli kuwa taaluma ya sheria imepanuka na masuala mapya kama vile
mafuta, gesi, haki bunifu na makosa ya kimtandao yamekuwa yakijitokeza kila
kukicha,” amesema.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) wakati akizungumza na wageni
mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu amesema uzinduzi wa ofisi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. John
Pombe Magufuli ya kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma. “Uzinduzi wa Ofisi unakamilisha
uwepo wa mihimili yote mitatu hapa Dodoma. Mahakama Kuu imetengewa ekari 50 na Ofisi
za mabalozi zimetengewa ekari 1,800; na wanatakiwa kuanza ujenzi mara moja,” amesema.
Amesema
ofisi hizo ni matokeo ya juhudi za makusudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anazochukua katika kuboresha mfumo wa
utoaji haki nchini na kuimarisha ulinzi wa maliasili na utajiri wa Taifa kwa kuunda
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
“Uamuzi
huu wa Mheshimiwa Rais unalenga kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata haki
zao kwa wakati na pia maslahi na heshima ya nchi vinalindwa kikamilifu,”
amesema.
Akizungumzia kuhusu
kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Waziri Mkuu amesema ni matarajio ya
kila mwananchi kuwa ofisi hiyo itapanua zaidi wigo wa utendaji wake hadi
kufikia ngazi ya wilaya.
“Binafsi
naamini kuwa, huu ni wakati muafaka wa kuongeza kasi ya kutekeleza dhana ya
utenganishaji wa shughuli za mashtaka na upelelezi. Hatua hii, itapunguza kama
siyo kuondoa kabisa malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya kubambikiziwa
kesi vinavyodaiwa kufanywa na vyombo vya upelelezi. Ofisi hii inategemewa kuwa
mkono wa Serikali katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji wa kesi
vinakoma na kuhakikisha kuwa kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi wa
kutosha,” amesisitiza.
Kuhusu
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali ndiyo mtetezi na mlinzi namba moja wa haki za Serikali na umma wa
Watanzania kwa ujumla wake na inapaswa kuhakikisha kuwa maslahi ya nchi
yanalindwa katika kesi zote za madai ambazo Serikali inashtaki au kushtakiwa
ndani na nje ya nchi.
“Ofisi hii inategemewa kuwa itajizatiti kujenga
ubobezi kwenye maeneo ya uendeshaji wa kesi za madai na usuluhishi ili
kuhakikisha kuwa inashiriki kikamilifu na tena kwa weledi katika kuendesha kesi
za madai ndani na nje ya nchi. Kujengwa kwa ubobezi katika ofisi hii,
kutalisaidia Taifa kuokoa fedha nyingi ambazo wakati mwingine Serikali hutumia
kuwalipa mawakili wa kigeni hususan katika mashauri ya usuluhishi nje ya nchi,”
amesema.
Akizungumza kuhusu ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Waziri Mkuu amesema mabadiliko ya kimuundo yaliyofanywa na Rais Magufuli
hayana budi kuwa chachu kwa ofisi hiyo ili iweze kuishauri Serikali katika
masuala ya kisheria hususan yale yanayohusu mikataba.
“Kama ilivyo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nayo
inategemewa kuwa itajenga ubobezi katika maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kutoa
ushauri mzuri kwa Serikali,” ameongeza.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema anaunga mkono uamuzi wa
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi wa kutaka kuwepo na
kanzidata ya wanasheria wote waliopo nchini ili waweze kutambulika kwa urahisi.
“Pia endeleeni na mpango wa kuwapangua
wanasheria kama mlivyojipanga, hii itasaidia kuleta ubobezi kwenye maeneo yao.
Pia sheria zibadilishwe na kuwekwa kwenye Kiswahili ili wananchi wazielewe kwa
urahisi,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, AGOSTI
15, 2018.
No comments:
Post a Comment