Mwakilishi
wa Kuehne Foundation Tanzania, Beatrice Millu (kulia), akimkabidhi
cheti, Paul Kuyi, mmoja wa washiriki wa mafunzo ya huduma kwa wateja,
utaratibu wa manunuzi na kupima utendaji kwa maofisa wa ulinzi, madini na
halmashauri mbalimbali na kufanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. (Picha na Francis Dande).
Picha ya pamoja.
Mratibu wa mafunzo hayo, Dk. Omari Swalehe akiwa na Mwakilishi
wa Kuehne Foundation Tanzania, Beatrice Millu.
NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam,
ikishirikiana na Taasisi ya Kuehne, wametoa mafunzo ya huduma kwa wateja,
utaratibu wa manunuzi na kupima utendaji kwa maofisa wa ulinzi, madini na
halmashauri mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya siku tatu,
Mkuu wa chuo hicho kampasi ya Dar es Salaam, Profesa Prosper Ngowi, alisema
lengo la mafunzo hayo ni kuboresha utendaji wa maofisa wa ngazi tofauti ili
kupata matokeo bora hasa kwenye utendaji wa kila siku.
Alisema taasisi ya Kuehne inalenga kuwapa watendaji na
wasomi hamasa ya kufanyakazi kwa kujituma huku wakijipima na kutarajia matokeo
chanya kwa maendeleo ya nchi.
“Mkitumia vizuri semina hii mtaonesha mabadiliko kwenye
utendaji wenu… hilo hasa ndio lengo la Kuehne kuona maendeleo kwenye utendaji
wa maofisa wa ngazi tofauti,” alisisitiza Profesa Ngowi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa kampasi, taasisi hiyo pia
inawawezesha wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo katika maeneo tofauti.
Mratibu wa semina hiyo, Dk. Omari Swalehe, alisema hiyo ni
semina ya tatu kufanyika chini ya ushirikiano wa Kuehne na Chuo Kikuu Mzumbe na
kwamba matokeo yanapimwa kwa utendaji wa wanufaika wa semina hizo.
Alisema mradi huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2016
utamalizika mwaka 2019 ukiacha alama ya mafaniko na maendeleo kwa watendaji wa
serikali na wasomi.
“Tunauhusiano ambao tunatoa semina kwenye eneo la ‘logistics’
hii ni ya tatu hapa Mzumbe, ya kwanza tulijadili kuhusu Kilimo na Uhifadhi wa Chakula
Ghalani wakati semina ya pili tulizungumzia kuhusu dawa za binaadamu, vifaatiba
na miundombinu ya kuzifikisha kwa wananchi.
“…Hii ya tatu tunajadili masuala ya utaratibu wa mnanunuzi
na huduma kwa wateja kwa watoa huduma kutoka taasisi za ulinzi, madini na
halmashauri mbalimbali hapa nchini,” alisema Dk. Swalehe na kuongeza kwamba
wanajadili namna sahihi ya kutoa huduma bora kwa wateja.
Alisema chini ya mradi huo wanafunzi wanakwenda kujifunza
kwa vitendo kwenye makampuni na mashirika makubwa yakiwemo ya saruji ili kuona
namna uzalishaji unavyofanyika.
Akizungumzia semina hiyo, Mwakilishi wa Taasisi ya Kuehne
hapa Tanzania, Beatrice Millu alisema lengo la semina hizo ni kuwaandaa wasomi
kufanyakazi kwa mpangilio wenye kuleta matokeo chanya.
“Kwa Afrika tunafanyakazi kwenye nchi 12 Tanzania ikiwemo na
tulianza rasmi mwaka 2010 kwa kusaidia Logiostics kwa Mashirika yanayohudumia
binaadamu na matokeo mazuri tumeyaona.
“...Hapa tunashirikiana na vyuo vikuu vya Mzumbe na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam tunaegemea zaidi kwenye Logistics na Supply Chain,
tunataka ifike mahali msomi anayehitimu kwenye vyuo hivyo awe na standard za
kimataifa yaani sawa na mhitimu wa Havard tunapandisha hadhi ya elimu Tanzania,”
alisisitiza Millu.
Kwa mujibu wa Millu, taasisi yake inataka kuona wanafunzi
wakipata elimu kwa vitendo zaidi kuliko nadharia kama ilivyo sasa huku
akisisitiza kwamba huo ni mradi wa miaka mitatu.
Mwisho…
No comments:
Post a Comment