Chama cha Skauti Tanzania tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini na kuafiki kuwa Mlezi wa Chama na kumuapisha Skauti Mkuu Mwantumu B. Mahiza.
Shukrani zetu kwa Mheshimiwa Rais kwa kuthamini mchango unaotolewa na wanachama pamoja na Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania.
Shukrani zetu zingine ni kwa Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania, Mheshimiwa DK. Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa awamu ya pili kwa mchango wake mkubwa kwa Chama cha Skauti, yeyé pamoja na Wadhamini wenzake DK. Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu mstaafu, na Askofu Nestori Timanywa (Marehemu) wamefanya kazi kubwa sana kuifikisha Skauti hapa tulipo.
Daima tutaendelea kuwaenzi Viongozi wetu kwa kulinda Heshima zao kwa kuwajibika na kufuata maelekezo yote watakayoyatoa kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.
Aidha tumehamasika sana na kufarijika na kauli ya Mlezi wetu kuwa anatambua shughuli za Skauti katika Taifa letu na kuthibitisha kuwa anafahamu changamoto zinazokabili Chama na kuahidi kuzishughulikia kwa uwezo wake wote na kwamba yupo pamoja nasi bega kwa bega.
Tunapenda kuwashukuru Viongozi wetu wote wa Kitaifa, kuanzia Mlezi, Wadhamini, Rais wa Chama cha Skauti, pamoja na Makamu Rais wa Chama. Skauti Mkuu, Wajumbe wa Bodi, Makamishna Wakuu Wasaidizi Makao Makuu, pamoja na Makamishna wote wa Skauti wa Mikoa na Wilaya zote Tanzania kwa kuratibu na kusimamia program za vijana skauti siku hadi siku.
Tunashukuru sana umma wa Watanzania hasa wazazi na walezi wa vijana skauti kwa kushirikiana nasi na kutuamini kuwalea watoto wao na vijana kwa kuwafundisha kuwa Wazalendo, Wakakamavu na wenye maadili mema ili kupata TAifa bora lenye Viongozi Wazalendo wenye kuipenda Nchi yao.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU KIBARIKI CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA.
ELINE KITALY
KAMISHNA MTENDAJI.
No comments:
Post a Comment