WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema changamoto ya upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana imeanza
kupungua nchini baada ya viwanda vingi kuanza kufanya kazi.
Serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria
kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda
ifikapo mwaka 2025.
Aliyasema
hayo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 6, 2018) alipotembelea kiwanda cha
kukoboa kahawa cha BUKOP na cha kusindika kahawa cha Tanica, mjini
Bukoba.
Alisema
kwa sasa tabia ya vijana wengi kukaa vijiweni imepungua kwenye maeneo
mengi nchini baada ya wengi kuajiriwa katika viwanda mbalimbali
vilivyoanzishwa na kufufuliwa.
Waziri
Mkuu alisema viwanda vimekuwa vikitoa ajira nyingi kwa wananchi, ambapo
alitolea mfano kiwanda kimoja cha Tanika kilichoajiri watumishi 800.
“Nyie
mlioajiriwa kiwandani hapa hakikishe mnafanya kazi kwa bidii, weledi,
uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili kukiwezesha kiwanda kuendelea na
uzalishaji,” alisisitiza.
Waziri
Mkuu ambaye yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku nne, inayolenga
kufuatilia maendeleo ya viwanda na zao la kahawa, ambalo ni kati ya
mazao makuu sita ya biashara.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Bukoba Bw. Bernad Limbe kuhakikisha anatafuta eneo kwa ajili ya
wafanyabiashara ndogondogo.
Aliyasema
hayo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa wakifanya
biashara katika eneo bandari na kuondolewa bila ya kupewa eneo lingine.
Waziri
Mkuu alisema ni marufuku kuwaondoa wananchi katika maeneo yao ya
kufanyia biashara bila ya kuwaonesha eneo lingine ambalo watalitumia
kwa aliji ya kufanyia biashara zao.
Awali,
Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Linus Leopord alisema kwa mwaka
wanazalisha tani 600 za kahawa iliyokaangwa na kusagwa, ambayo
inatosheleza kwa mahitaji ya soko.
Pia
kiwanda cha kahawa cha Tanica kinauwezo wa kuzalisha kahawa ya unga
tani 500 kwa mwaka ila kutokana na uchakavu wa miungombinu kinazalisha
tani 300 kwa mwaka.
Kuhusu
masoko Bw. Leopord alisema kwa sasa mauzo yameongezeka, wanauza tani 50
ya kahawa iliyokaangwa na kusagwa kwa mwezi, ambapo awali walikuwa
wanauza tani 32.
Kadhalika,
Meneja huyo alisema wameimarisha na kuongeza soko la nje ambapo kwa
sasa wanauza tani 35 za kahawa ya unga kwa mwezi, awali walikuwa wanauza
tani 20.
Alisema
kiwanda cha Tanika kinamilikiwa na chama cha ushirika cha KCU (53.37
%), KDCU (31.8%), Hazina (7.67), TFC (6.22%) na wafanyakazi wa Tanica
(0.92%).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 7, 2018.
No comments:
Post a Comment