WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi
awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa
kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi jirani akiwemo Mkuu wa
Polisi wa Wilaya hiyo, Justin Joseph.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 7, 2018) baada ya kukagua kiwanda cha
kukoboa kahawa cha Nkwenda wilaya Kyerwa katika siku ya pili ya ziara
yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameambatana
na Mkewe Mama Mary Majaliwa.
“Askari
polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza
kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi ya jirani kupitia
njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na
Omukatoma.”
Waziri
Mkuu amesema ni jambo la hatari kama askari Polisi wanasindikiza kahawa
inayouzwa kwa magendo, hivyo ameagiza jambo hilo lidhibitiwe
haraka.”Marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na
polisi msishiriki katika butura.”
Katika hatua nyingine,Waziri
Mkuu amesema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa
inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya
kufanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waziri
Mkuu amesema minada yote ya kahawa ikifanyika mkoani Kagera
itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa muda mfupi na pia itapunguza
makato yasiyokuwa ya lazima ambayo ni kero kwa wakulima.
“Wanunuzi
watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa
fedha zake kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji
utamuwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni
rahisi mkulima kuibiwa.”
Waziri
Mkuu amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ambayo
imedhamiria kuwaletea maendeleo na kwamba itahakikisha kila mmoja
anapata haki yake wakiwemo wakulima ambao watasaidiwa katika kutafutiwa
masoko ya mazao yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 7, 2018.
No comments:
Post a Comment