HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2018

Msaga Sumu atikisa Tamasha la Nyerere

NA MWANDISHI WETU, MKURANGA

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Selemani Jabir maarufu kwa jina la ‘Msaga Sumu’, juzi Jumapili alikonga nyoyo za mashabiki kwa nyimbo zake za utamaduni wa Kiswahili katika Tamasha la kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika viwanja vya Kisemvure, Mkuranga mkoani Pwani.
 
Msaga Sumu alialikwa na Mratibu wa Tamasha hilo, Ahmed Salim, ambako alitumia fursa hiyo kuwaunganisha watu wa Mkuranga kwenye tamasha hilo lililohudhuria maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo pamoja na vitongoji vyake. 
 
Msaga Sumu ambaye ni mwanamuziki mahiri wa nyimbo za uswahilini, alitamba katika tamasha hilo na nyimbo kadhaa zikiwamo ‘Iga Tena’, ‘Matobo’, na ‘Kitu Gani’, ambako aliteka umati uliohudhuria na kuacha gumzo.
 
Mratibu wa tamasha hilo, Ahmed Salim alisema kilichomsukuma kuandaa tamasha hilo ni kuenzi upendo wa dhati wa Mwasisi wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
 
“Upendo ule na Mwalimu ambao haukuwa na chembe ya ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, matokeo yake ni amani tuliyonayo hapa nchini inayoenziwa na Rais John Pombe Magufuli. Ni mshikamano na tunu yetu sasa,” alisema Salim.
 
Alisema kwamba tamasha hilo litabeba ujumbe tosha kwa wananchi kuenzi yale yote yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa shabiki na mchezaji mkubwa wa bao–michezo ambayo siku hiyo ilichezwa kwa umahiri pamoja na michezo ya kuvuta kamba, kukimbiza kuku na mbio za pole ambayo Nyerere aliitumia kama kuenzi umamani upendo na mshikamano.
 
Naye, Pembe Mlekwa, Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani alisema kwamba Mkurunga itaendelea kumuenzi Mwalimu kwa vitendo na kukumbushana kupitia matamasha hayo.
 
“Napenda kukumbusha umma kuwa kuwa siku hii si ndogo. Tutaendelea kudumisha siku hii kwa ajili ya amani ya nchi yetu,” alisema Mlekwa aliyesisitiza watu kujisomea vitabu vingi vilivyoandikwa na Mwalimu.

No comments:

Post a Comment

Pages