NA SALUM MKANDEMBA
WAKATI
Kampuni Bora 100 za Mwaka 2018/19, zikitarajiwa kutangazwa leo, Benki ya NMB
imesema itaongeza kiwango cha mikopo inayoitoa kwa kampuni ndogo na za kati
mara mbili na kufikia Shilingi trilioni 3 kwa miaka mitatu ijayo.
Hayo
yalisemwa na Mkurugenzi Mtengaji wa NMB, Ineke Bussemaker, wakati akizungumzia
udhamini wa NMB kwa hafla ya Kampuni Bora 100 za Mwaka 2018/19 (Top 100
Mid-sized Companies' Survey).
Kwa
miaka mitatu iliyopita, NMB imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni
1.5 kwa kampuni ndogo na za kati, ambako Bussemaker alisema kampuni
zinazowekeza katika kufanya biashara kijiditali zipo katika nafasi nzuri zaidi
ya kufanya vizuri kibiashara.
"Hatima
ya uchumi wa nchi upo katika kufanya biashara kidijitali ili kuhakikisha mifumo
ya utendaji inakwenda kwa kasi,” alisema na kuongeza kuwa kampuni zilizoweza
kuweka mifumo sawa ya dijitali zipo katika nafasi bora zaidi ya kupata mikopo
kutoka katika benki yake.
Alisema
NMB inazidi kuwekeza katika mifumo ya utoaji huduma kwa njia za kidijitali ili
kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma zake nchini kote.
Kampuni
Bora 100 Tanzania ni shindano linaloendeshwa na Mwananchi Communications
Limited kwa kushirikiana na KPMG, ambapo mbali na NMB, wadhamini wengine ni
pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Azam Media na Hoteli ya Hyatt
Regency.
Akitoa
matokeo ya utafiti wa Kampuni Bora 100 za Mwaka 2018/19, Mtafiti Kiongozi wa Kampuni
ya AZ Advisory, Dk. Remidius Ruhinduka, alisema asilimia 23 ya Kampuni za kati
nchini zinaona mwenendo wa uchumi nchini kwa kipindi cha miezi sita iliyopita
sio mzuri.
Mkutano
huo wa utafiti umefanyika ikiwa imesalia siku moja kufikia fainali za Shindano
la Top100 ambayo inafanyika leo, katika fainali hizo kampuni bora 100 za kati
zitatangazwa.
Dk
Ruhinduka alisema asilimia kubwa ya wafanyabiashara wana matumaini ya kuimarika
kwa uchumi licha ya changamoto walizonazo katika biashara zao.
"Mtazamo
wa wafanyabiashara kwa kipindi cha miezi 6 iliyopita asilimia 55 wanasema
biashara inaimarika, asilimia 22 wanasema iko sawa na asilimia 23 wanasema
mwenendo sio mzuri.
“Hata
hivyo kwa kipindi cha miezi sita ijayo, asilimia 60 wanasema uchumi utaimarika,
asilimia 28 utakuwa sawa na asilimia 12 itakuwa mbaya," amesema Dk.
Ruhinduka.
No comments:
Post a Comment