NA TIGANYA VINCENT, RS TABORA
WAFANYABIASHARA na
Wajasiriamali wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kutumia kikamilifu Jukwaa la
Biashara na Uwekezaji lijalo mkoani humo kutangaza fursa za biashara na
uwekezaji ili waweze kuinua na kupanua wigo na mitaji yao.
Kauli hiyo imetolewa
jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa mkutano wa hadhara uliolenga
kuwatangazia wananchi, wafanyabiashara na Wajasiriamali wa Mkoa juu ya Jukwaa la
Biashara na Uwekezaji litakalofanyika mwishoni mwa Mwezi ujao.
Alisema Jukwaa hilo ni
fursa nzuri kwa wakazi wa Tabora na hasa wafanyabiashara na Wajasiriamali kuongeza mtandao wa biashara kati
yao na wale wa kutoka nje ya Mkoa huo kupitia utangazaji wa bidhaa zao na fursa
zilizopo za uwekezaji.
Mwanri alisema hatua
hiyo itawasaidia kuwafanya kuwa wachangia katika fursa za uwekezaji na biashara mkoani humo na sio kuwaacha kama
watazamaji wa watu kutoka nje kuja kunufaika pekee yao.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa
aliwataka wamiliki wa Hoteli na Nyumba za kulala wageni , Madereva bodaboda na
vyombo vingine vya usafiri kuhakikisha wanakuwa wakarimu na kutoa huduma ambayo
itawafanya washiriki wa Jukwaa hilo watamani kuwekeza Tabora.
Alisema wananchi wa
Tabora wanatakiwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani humo
kuwafichua waharifu ili kuweka mazingira mazuri ambayo yatawafanya watu wenye
nia ya kuwekeza kuwa na uhakika wa usalama wa uwekezaji wao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Tabora Kitwala Komanya aliwataka watu wenye nia ya kuwekeza kwenda Tabora kwa
sababu ya kufunguka kwa miundombinu muhimu ya kuvutia ikiwemo barabara za lami zinaunganisha Mkoa huo na
mingine, mradi wa maji kutoka ziwa Victoria na Uwanja wa Ndege unaoruhusu ndege
kubwa kutua masaa 24.
Aidha Mkuu huyo wa
Wilaya alisema katika kuhakikisha Manispaa ya Tabora inaendelea kuwa mahali
salama pa kuwekeza ameliagiza Jeshi la Polisi kuendesha Doria la kukapambana na
majambazi , vibaka na waharifu wengine.
Alisema lengo ni
kuhakikisha Tabora inakuwa sehemu mfanyabiashara ataendesha shughuli zake bila
hofu na mashaka ya kuvamiwa.
No comments:
Post a Comment