HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 11, 2018

RC Wangabo awatahadharisha Wakurugenzi na Madiwani kuhusu mapato

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wakurugenzi wa halmashauri pamojana waheshimiwa madiwani juu ya kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kufikia malengo zaidi ya waliyowekewa na Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.


Wizara ya OR – TAMISEMI imesema kuwa itawapima wakurugenzi kulingana na makunsanyo ya mapato yao na kuwataka hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2018/2019, halmashauri zimetakiwa kufikia asilimia 81 ya ukusanyaji wa mapato.

Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa Mh. Wanagbo amewaomba waheshimiwa madiwani kuhakikisha kila vikao vyao vinapofanyika agenda ya mapato ipewe kipaumbele na kuwang’ang’ania wakurugenzi na kuwawajibisha wale wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kwani wao ndio chanzo cha kupata sifa mbaya.

“Waswahili wanasema ‘mchelea mwana kulia hulia yeye’ sasa kama tutawalealea hawa ambao wanatusababishia sisi tusikusanye mapato matokeo yake mkichelea kwenu nyinyi kama viongozi na wawakilishi wa wananchi mtakuja kuhukumiwa kule kwenye kura, “Alisema.

Ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika mwezi huu wa nane katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa ikijumuisha wadau mbalimbali wa maendeleo, Wabunge, Madiwani, Viongozi wa dini na wataalamu wa Halmashauri na sekretarieti ya mkoa.

Aidha, alizipongeza Halmashauri ambazo zimevuka lengo la makusanyo lililowekwa na Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Halmashuri mbili za Wilaya ya Nkasi pamoja na Wilaya ya Sumbawanga zilikusanya kwa asilimia 90, huku Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ikiwa imekusanya kwa asilimia 63 na Manispaa ya Sumbawanga ikiwa imekusanya asilimia 53. 

IMETOLEWA NA OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment

Pages