HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2018

WAANDISHI WA HABARI ZA KILIMO SAYANSI WAPIGWA MSASA JIJINI DODOMA

Mwanaharakati na Mwandishi wa Vitabu kuhusu Sayansi ya Kilimo kutoka nchini Uingereza Mark Lynas (kulia), akitoa mada kwenye mafunzo ya uandishi wa habari za kilimo  Sayansi kuhusu Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) kutoka mikoa mbalimbali na nje ya nchi yaliyofanyika jijini Dodoma leo.
 Mafunzo yakiendelea.
 Mratibu wa OFAB nchini Tanzania, Dk.Philbert Nyinondi, akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
 Mtafiti wa Kilimo, Justin Ringo,  kutoka Kituo cha Utafiti cha TARI-Ilonga mkoani Morogoro, akichangia jambo.
 Mwanahabari Dino Mgunda akichangia jambo.
 Mwanahabari David Rwenyagila akichangia jambo.
 Mwanahabari Benson Eustace akiuliza swali. 
 Mafunzo yakiendelea.

 Ofisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Thomas Chali, akielezea kuhusu kanuni za matumizi ya GMO hapa nchini.
Mhariri Mtendaji wa Taasisi ya Cornell Alliance for Science Bi. Joan Conrow kushoto), akielezea jinsi ya kuandika habari zinazohusu GMO. Kulia ni Mwanaharakati na Mwandishi wa Vitabu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira kutoka nchini Uingeleza Bw.  Mark Lynas.


Na Dotto Mwaibale, Dodoma

WAANDISHI wa Habari nchini  wametakiwa kutumia taaluma zao kuelimisha jamii kuhusu  Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) hasa katika sekta ya kilimo.

Akitoa mada katika mafunzo  kwenye mafunzo ya uandishi wa habari wa kilimo sayansi kuhusu GMO kutoka mikoa mbalimbali na nje jijini Dodoma leo Ofisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Thomas Chali alisema waandishi wa habari ni wa muhimu katika kutoa mafunzo kupitia taaluma zao.

Katika hatua nyingine Chali alisema pamoja na kuwepo kwa Sheria ya uwepo Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) nchini bado zipo changamoto kuu tano katika usimamizi wa teknolojia hiyo ya kisasa.

Alisema Sheria ya Tanzania inaruhusu matumizi na kufanyika kwa tafiti mbalimbali zinazohusu GMO ila kinachohitajika ni taratibu kufuatwa ili kuhakikisha usalama unakuwepo.  

Alisema pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo changamoto ya uelewa mdogo, uchache wa wataalam, uhaba wa miundombinu, uwepo wa mfumo wa uwajibikaji na wasiwasi wa baadhi ya watu ni mambo ambayo wanayafanyia kazi ili kuhakikisha tekonolojia hiyo inakuwa na manufaa nchini na kwa wananchi.

Ofisa huyo alisema ili kuhakikisha wanaenda pamoja katika kutatua changamoto hiyo wamekuwa wakitoa elimu, kuwajengea uwezo watu mbalimbali kuhusu teknolojia hiyo.

Chali alisema Serikali inatambua fursa zilizopo katika matumizi ya bioteknolojia ya kisasa kwenye kuendeleza sekta ya kilimo nchini ambayo ni mkombozi wa wananchi kwa asilimia kubwa.

Akichangia Mada kuhusu GMO, Mwanaharakati na Mwandishi wa Vitabu kuhusu Sayansi ya Kilimo kutoka nchini  Uingereza,Mark Lynas   alisema waandishi wa habari ni watu muhimu katika  mafanikio ya jamii yeyote hivyo wanawajibu wa kutumia taaluma yao kuwabadilisha na kuelezea teknolojia hiyo ya kisasa.

"Mimi ni mmoja ya watu ambao nilikuwa napinga GMO lakini baada ya kupata elimu ya kutosha nikaelewa na sasa nimekuwa mwanaharakati mzuri ambaye nimeandika vitabu vya kilimo sayansi,"alisema.

Alisema GMO  kwa sasa imethibitishwa na taasisi na mashirika mbalimbali  duniani kama American Association for the Advancement Science (USA), National  Academia of Science (USA), Royal Society (UK), African Academia of Science na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa haina madhara  katika  kilimo.

Mwanaharakati  huyo alisema kwa sasa bidhaa za GMO  zinatumika kwa binadamu na mifugo kote duniani hivyo  hakuna namna ya kuikwepa.

Aidha Mwandishi huyo alisema GMO  inaonesha matokeo chanya kwa wakulima ambapo wanavuna mazao kwa asilimia 200 tofauti na awali.

Pia aliongeza kuwa teknolojia hiyo imekuwa mkombozi katika maeneo yaliyoathirika kwa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Lynas alisema hoja za baadhi ya watu kuwa GMO inasababisha magonjwa ya saratani na vichwa vikubwa haina mashiko katika ulimwengu  wa sasa.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Jukwaa la Wazi la Kilimo na Teknolojia Afrika (OFAB) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani, Cornell Alliance for Science na African Agricutural Technology Foundation (AATF). 

No comments:

Post a Comment

Pages