HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA MRADI WA MAJI CHATO UKAMILIKE KWA WAKATI

*Ni wa Imalabupina/Ichwankima wenye thamani ya sh. bil. 8.28

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaameweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Imalabupina/Ichwankima wilayani Chato ambao una thamani ya sh. bilioni 8.28 na amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo wahakikishe unakamilika kwa wakati.

Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Novemba 27, 2018) alipozungumza na wananchi kwenye kijiji cha Nyamirembe baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa maji wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Geita.

Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote nchini wakiwemo na wa wilaya ya Chato mkoani Geita wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao, hivyo amewataka waendelee kuwa na imaji na Serikali yao.

“Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo mbalimbali nchini vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Chato ili kuwawezesha wananchi kupata maji.”

Waziri Mkuu ameagiza mradi huo ukamilike kwa wakati kwa kuwa Serikali inahitaji kuona wananchi wakinufaika na huduma hiyo. Mradi huo ulianza kujengwa Mei, 2017 na ulitakiwa ukamilike Mei, 2018 ila kutokana na changamoto mbalimbali unatarajiwa kukamilika Februari 2019.

Awali,Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi, Mtemi Simeon alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia watu takribani 59,609 katika vijiji 11 vilivyopo kwenye kata nne za Nyamirembe, Ichwankima, Kachwamba na Kasenga.

“Vijiji vitakavyonufaika na mradi huu ni Nyamirembe, Kalebezo, Nyambiti, Busalala, Imalabupina, Ichwankima, Kachwamba, Ipandikilo, Idoselo, Igagula na Mwangaza. Tayari vituo 240 vya kuchotea maji vimeshakamilika na matenki nane kati ya tisa yamekamilika pamoja na mabirika 10 ya kunyweshea mifugo.”


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, NOVEMBA 27, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages