*Ni baada ya wanafunzi 72 wa kike kupewa ujauzito wilayani Nyang’hwale
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amechukizwa na vitendo vya watoto wa kike
kukatisha masomo yao kwa kupata ujauzito wilayani Nyang’hwale ambapo
jumla ya wanafunzi 72 wamepata ujauzo katika kipindi cha miaka mitatu
cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.
Kutokana
na wilaya hiyo kuwa na idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokatisha
masomo kutokana na ujauzito, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa wilaya ya
Nyang’hwale Hamim Gwiyama kufanya operesheni katika kila kijiji na
kubaini waliowapa wanafunzi ujauzito na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatano, Novemba 28, 2018)
alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa Sabasaba, ,kijiji cha Kalumwawilaya ya Nyang’hwale, akiwa katika ziara yake mkoani Geita.
“Jambo
lingine litakalowawezesha kukabiliana na tatizo la ujauzito kwa
wanafunzi wa kike ni kuanzisha miradi ya ujenzi wa mabweni ili watoto wa
kike waweze kusoma bila ya kupata vishawishi vinavyosababisha wao
kupata ujauzito.”
Waziri
Mkuu alisema Serikali haiwezi kuacha jambo hilo likiendelea, hivyo
aliwataka wananchi washirikiane katika kuwalinda watoto wa kike na Serikali itawachukulia hatua watendaji wote ambao katika maeneo yao watoto wa kike watabainika kuwa na ujauzito.
“Watoto
wa kike lazima waheshimiwe waachwe wasome bila ya usumbufu na
atakayekatisha masomo adhabu yake ni kali. Tukikukuta umesimama na binti
katika kona isiyoeleweka tutakukamata. Ole wenumtakaobainika kuwapa ujauzito wanafunzi, adhabu yake ni miaka 30 jela.”
Waziri
Mkuu pia, alitoa onyo kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike
ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto
wao wa kiume kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za
kisheria.
Katika
kuoneshwa kuchukizwa na jambo hilo, Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI, Mwita Waitara ambaye anashughulikia elimu, amemueleza
Waziri Mkuu kwamba Novemba 30, 2018 yeye arudi wilayani hapo kwa ajili
ya kuwashughulia wote wanaokatisha masomo wanafunzi kike. Ametoa namba
ya simu ili wananchi waanze kumpa taarifa za wahusika.
Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu alisemaSerikali imedhamiria kusambaza
umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo
nchini vitaunganishiwa katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini
(REA).
“Rais
wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata
umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza
kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa
umeme huo ni sh. 27,000 tu.”
Kuhusu
suala la gharama za kulipia nguzo, Waziri Mkuu alisema wananchi
hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo pamoja na zile za
fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo
zimeshabebwa na Serikali.
Awali,
Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Nyamigogo
ambapo alikagua miundombinu ya kiwanda hicho na kisha aliweka jiwe la
msingi la ujenzi wa kiwanda hicho, ambacho muwekezaji wake ni mzawa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, NOVEMBA 29, 2018.
No comments:
Post a Comment