HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 03, 2018

AMDT YAWATAKA WAKULIMA WA ALIZETI MKOANI MANYARA KUCHANGAMKIA FURSA

Kaimu Katibu tawala mkoa wa Manyara,Anza Amen Ndosa akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) walipotembelea ofisi ya mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kuangalia namna AMDT inawezesha wakulima wa Alizeti kupitia miradi yake..kulia kwake ni Afisa Kilimo wa mkoa huo, Norbert Emmily .
Mkurugenzi Mtendaji  wa taasisi ya  Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) ,Michael Kairumba akitoa taarifa kwa Wajumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo namna ambavyo AMDT imekuwa ikiwawezesha wakulima wa zao la Alizeti kupitia miradi yake.
Afisa Kilimo mkoa wa Manyara ,Norbert Emmily akitoa taarifa kuhusu kilimo cha zao la Alizeti katika mkoa huo kwa Wajumbe wa Bodi ya  Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) walipotembelea ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Mkurugenzi wa kampuni ya Quality Food Product (QFP) Sherry Woodring ambaye ni Mdau wa Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) akitoa taarifa mbele ya Wajumbe wa Bodi ya taasisi hiyo kuhusu zao la Alizeti katika mkoa wa Manyara .
Mkurugenzi wa kampuni ya Quality Food Product (QFP) Sherry Woodring ambaye ni Mdau wa Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) akitoa maelezo kwa  Wajumbe wa Bodi ya taasisi hiyo walipotembelea kiwanda cha kukamulia Alizeti kilichopo mkoani Manyara.
Sehemu ya Mitambo iliyopo katika kiwanda cha Kukamulia Alizeti kilichopo mkoani Manyara.
Magunia ya Alizeti yakiwa katika kiwanda cha kukamua Alizeti cha Agro. 
Meneja Mradi wa Alizeti kutoka  Taasisi ya kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) Martin Mgallah akizungumza wakati Wajumbe wa Bodi ya taasisi hiyo walipowatembelea wakulima wa zao la Alizeti katika kijiji cha Mwada mkoani Manyara.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii .
Babati Manyara.

TAASISI ya Kuendeleza Mifumo ya Kimasoko ya Kilimo- Tanzania (AMDT), imewataka wakulima wa zao la Alizeti mkoani Manyara kuachana na kilimo cha mazoea cha zao hilo na badala yake waelekeze nguvu katika kilimo cha kibiashara kwa kutumia pembejeo bora hasa mbegu na kufuata mbinu bora za ugani ili kuongeza tija kwenye mavuno na hivyo kukuza vipato vyao.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mradi wa Alizeti unaosimamiwa na Taasisi ya AMDT, Martin Mgallah wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi wa taasisi hiyo waliyoifanya hivi karibuni mkoani Manyara.
Katika ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kujifunza na kuona mafanikio pamoja na changamoto za utekelezwaji wa mradi wa kilimo cha Alizeti kwa wakulima wa Mkoa wa Manyara, Bwana Mgallah alisema toka kuanzishwa kwa mradi huo, pamekuwepo na mwitikio chanya kutoka kwa wakulima wengi kushawishika kujikita kwenye kilimo cha zao la Alizeti.

Hata hivyo Bwana Mgallah ameongeza kuwa licha ya mapokeo chanya bado hitaji la zao la Alizeti kwa Mkoa wa Manyara ni kubwa na hivyo kufanya soko la mazao yatokananyo na alizeti kuwa kubwa ndani ya mkoa huo na mikoa mingine.

“Niwatoe hofu wakulima na hasa wanaoanza kulima zao hili kutoogopa kwani soko lake ni kubwa hapa Manyara lakini hata nje ya mkoa, masoko ni ya uhakika, Sisi kama AMDT tumedhamiria kutoa elimu kwa wakulima, kuwaunganisha na watoa huduma za msingi kwa kilimo na kuwasaidia kupata mbegu bora zililizoboreshwa zitakazo wawezesha kupata mazao kwa wingi,”alisema.

Mgallah amesema  iwapo wakulima watazingatia maelekezo ya wataalamu na matumizi ya mbegu bora basi Tanzania inaweza kuondokana na tatizo la uagizaji mkubwa wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, ambapo takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 60% ya mafuta hayo huagizwa toka nje ya nchi.

Kwa upande wake Kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Manyara Anza Amen Ndossa amesema katika mkoa wa Manyara zao la Alizeti ni moja kati ya mazao ya biashara ya kimkakati ambayo mkoa huo umekuwa ukihamasisha wakulima kujihusisha nao, kutokana na ardhi ya eneo lao kuruhusu kusitawi kwa zao hilo.

“Kilimo cha Alizeti ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo mkoa umekuwa ukihamasisha wakulima wetu kujihusisha nayo, Tunatambua mchango wake katika kuinua hali za Maisha za wananchi wetu, na ndio maana ujio wa wadau kama AMDT na QFP kwetu ni faraja maana mwisho wa siku utamsaidia mkulima wa hali ya chini kuweza kulima kwa tija na kuweza kujikwamua kiuchumi” Alisema Ndosa.

Kwa Upande wake Afisa kilimo wa Mkoa wa Manyara Bwana Norbert Emmily amesema toka kuanza rasmi kwa kilimo cha Alizeti mwaka 2000, wakulima wengi wamekuwa wakihamasika kujihusisha na kilimo hicho huku akitaja changamoto ya uhaba wa mbegu bora za Alizeti kuwa ni kikwazo kutokana na ukweli kwamba wakulima wengi wanatumia mbegu za asili, ambazo utoaji wake wa mafuta umetajwa kuwa wa chini ukilinganisha na mbegu Chotara.

Mkoa wa Manyara kwa sasa kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji wa zao hilo zinaonyesha kumekuwepo na ongezeko kubwa la tija kwa wakulima na hasa katika mavuno ambapo kwa sasa mkulima anapata wastani wa gunia sita mpaka gunia nane ukilinganisha na gunia mbili mpaka tatu mpaka nne kwa eka mnamo mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment

Pages