HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 04, 2018

Dk. Mengi akaribisha Wachina kuwekeza

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uhamasishaji Ushirikiano wa Nchi za Kusini kutoka China, Lyu Xinhua, wakati alipokutana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka China. (Picha na Francis Dande).


NA JANETH JOVIN

MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kushirikiana naye kufanya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kubangulia Korosho mkoani Mtwara.

Sekta zingine ambazo wawekezaji hao wamekaribishwa kuja kuwekeza nchini ni uchimbaji wa madini ya dhahabu, kukifufua kiwanda cha General Tyre cha mjini Arusha na ujenzi wa bomba la gesi kutoa Dar es Salaam hadi Uganda.

Dk. Mengi alitoa rai hiyo jijini Dar es Salaam jana alipokutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa 30 kutoka China waliokuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.

Alisema anawakaribisha wawekezaji hao hapa Tanzania kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo wasisite kuja kuwekeza.

Alisema mkoani Mtwara korosho zinapatikana kwa wingi lakini kuna uhaba wa viwanda vya kubangulia korosho hizo, hivyo kama wawekezaji hao kwa kushirikiana naye watawekeza kwenye ujenzi wa kiwanda wataisaidia Serikali na jamii kwa ujumla kutatua tatizo hilo.

Aidha Dk. Mengi aliwaeleza wawekezaji hao kuwa nchi ya Tanzania ina ardhi zuri yenye rutuba, rasilimali nyingi pamoja na madini mbalimbali kama vile dhahabu, almasi, Tanzanite na nyinginezo, hivyo anawakaribisha wawekezaji hao kuungana naye katika kufanya uwekezaji.

Naye balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Wang Ke alisema anamshukuru Dk. Mengi kwa kuwaalika wawekezaji hao na kuongeza kuwa ni mmoja wa wafanyabishara wakubwa waliofanikiwa Tanzania na amekuwa akiwasaidia watu mbalimbali wasiojiweza.

Alisema anatambua kuwa kampuni za IPP zilizochini ya Dk. Mengi zimekuwa na mchango mkubwa nchini Tanzania kutokana na kuwekeza kwenye sekta ya viwanda na kuajiri watu wengi.

"Kupitia ushirikiano huu wa Dk. Mengi uliyoanzishwa utakuwa na manufaa makubwa kwani ni vitu vinne ambavyo ametuabia kuwa tunaweza kushirikiana naye kufanya uwekezaji, " alisema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la uhamasishaji ushirikiano wa nchi za kusini kutoka China, Lyu Xinhua alisema kampuni 17 kutoka China zimekuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.

Alisema, kampuni hizo zimekuja kuangalia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali kama vile masuala ya uhandisi, mazao ya biashara, elimu, usafirishaji wa zao la korosho, teknolojia ya umeme na zinginezo.

Xinhua aliwakaribisha wawekezaji wengine kutoka China kuja Tanzania kufanya mazungumzo ya uwekezaji na Dk. Mengi kwani ni mtu ambaye amefanikiwa sana kwenye sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages