WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kuenzi misingi ya utawala bora haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma
atakayekiuka misingi hiyo na kutanguliza maslahi binafsi badala ya
maslahi ya umma katika utendaji wake.
Amesema
mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu
wachache huku wananchi wengi kuendelea kuwa fukara, wakati wachache
wakijitajirisha isivyo halali, hivyo Serikali itaendelea kuziba mianya,
kwani ikiachiwa iendelee, itarudisha nyuma jitihada za Serikali katika
kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema mmomonyoko wa maadili umechangia sana
kutozingatiwa kwa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali katika utumishi
wa umma, tatizo ambalo limesababisha mgongano wa maslahi.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Desemba 10) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku
ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma,
ambapo ametumia Napenda fursa hiyo kuwaasa viongozi wote kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wao kwani hiyo ndio njia
pekee itakayoepusha mgongano wa maslahi.
Waziri
Mkuu amesema mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia
kuisababishia hasara Serikali kwa muda mrefu, tatizo ambalo lazima
lidhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi au watumishi wa umma
wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi
binafsi nayo.
”Mathalan
katika Halmashauri zetu wapo madiwani au watumishi wanaoshiriki kutoa
maamuzi yanayohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati
kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa
rushwa.”
Amesema
mgongano wa maslahi ambapo amesema kuwa huwa unatokea pale mahitaji,
manufaa na faida (maslahi) binafsi ya kiongozi yanapokinzana na yale ya
umma katika utendaji wake wa kazi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya
utawala bora ambayo Taifa letu linaiamini na kuifuata tangu
lilipoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.”
Amesema
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kuunga
mkono na kutekeleza Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa ipasavyo.
Mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kupambana
na Rushwa na Makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa Haki za
Binadamu.
”Sambamba
na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika ibara
ya 145 (a), ambapo tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani,
mojawapo ya agenda yetu ilikuwa ni kuendeleza jitihada za kukuza,
kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria katika ngazi
zote za uongozi.
Jambo
hili tumelifanya kwa nguvu kubwa na kwa sasa tumeona kuna mabadiliko
makubwa sana miongoni mwa watumishi wa umma katika kutoa huduma kwa
wananchi kwa nidhamu, bila upendeleo na kuepuka vitendo vya rushwa.”
Waziri
Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitatu yameshuhudiwa mafanikio
makubwa nchini na kwamba hakuna muujiza uliofanyika kufikia hatua hiyo,
bali ni usimamiaji wa nidhamu ya kazi, uadilifu na rasilimali za nchi.
Amesema
kinachofanywa na Serikali ni kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo
vyote vinavyokiuka maadili na misingi ya utawala bora kadri
inavyowezekana na sasa mafanikio ya jitihada hizo yanaonekana, ambapo
baadhi ya watumishi wa umma waliishakuwa miungu
watu na kusahau kabisa kwamba utumishi wao ni wa kuwatumikia Watanzania,
”Mafanikio
ya hatua hizo ni kurejea kwa nidhamu katika utumishi wa umma, kushuka
kwa mfumuko wa bei za bidhaa, kuendelea kutekelezwa kwa miradi ya
maendeleo na kuimarika kwa utamaduni wa kufanya kazi halali ili kupata
kipato halali hivyo, kufuta maisha yaliyojaa ujanja ujanja.”
Hivyo,
Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yanatoa fursa
ya Serikali kujitathmini kama imefanya juhudi za kutosha kuhakikisha
maadili yamezingatiwa katika kila eneo na hivyo kupunguza vitendo vya
rushwa, kuimarisha uwajibikaji katika kuutumikia Umma na misingi ya
utawala bora kwa ujumla wake.
Maadhimisho
hayo yamehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni MstaafuGeorge Mkuchika, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi.
Wengine
ni Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu Wakuu wa Taasisi zinazosimamia
Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji na Mapambano dhidi ya Rushwa,
Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wawakilishi wa Washirika wa
Maendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma,
JUMATATU, DESEMBA10, 2018.
No comments:
Post a Comment