Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
Upanuzi wa
bandari ya Dar es Salaam umefikia hatua nzuri baada ya kukamilka kwa upanuzi wa
gati namba moja kwa asilimia 100 huku meli ya kwanza ikitarajiwa kutia nanga
wiki moja ijayo ikishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
Hayo
yameelezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),
Mhandisi Deusdediti Kakoko, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa Sh. bilioni 336.7 wa upanuzi
wa bandari hiyo.
Amesema
upanuzi huo umeiongezea uwezo gati hiyo yenye urefu wa mita 192 wa kubeba meli
kubwa mbili za tani 45,000 hadi tani 60,000 kwa wakati mmoja kutokana na
kuongezewa kitako cha upana wa mita 11.5 kinachobebwa na nguzo imara za zege
zilizochimbiwa mita 70 chini ya bahari.
Amesema
baada ya mkandarasi kukabidhi gati hiyo siku chache zijazo atakabidhiwa na kuanza kazi ya upanuzi wa gati namba mbili
inayotarajiwa kukamilika Machi mwakani na upanuzi utaendelea hadi kufikia gati
namba saba.
Akizungumzia
ujenzi wa gati ya magari (RoRo Berth) pamoja na yadi ya kuegesha magari amesema
mradi huo ulitakiwa uwe umekamilika lakini mkandarasi alikutana na changamoto ya
kuwepo kwa udogo mbaya na hivyo kulazimika kutafuta udogo mzuri na kuujaza na
kwamba ujenzi unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Juni mwakani.
Kakoko
amesema kukamilika kwa gati hiyo kutaiwezesha bandari hiyo kupokea magari
10,000 kwa siku kutoka uwezo wa kupokea magari 2500 na kwa mwaka itakuwa magari
200,000 kutoka magari 90,000.
"Kukamilika
kwa gati hii kutaleta mapinduzi makubwa kwani tunà weza kupokea meli ya magari
3000 hadi 5000 na ikapakuliwa kwa siku moja tu," amesema na kusisitiza;
"Ndugu
wananchi na wadau hasa mawakala wa meli wakae mkao wa kula waachane na siasa za
kuambiwa meli zina subiri sana hapa tuna meli 12 tu na zilishawahi kufika 18 tu
naomba wananchi wawe na amani serikali yao inafanya kazi."
Ameongeza
kuwa upanuzu wa gati utaenda sambamba na upanuzi wa lango la bandari kwa
kuongeza kina kutoka mita 10 hadi 16 ambapo kwa sasa unafanyika usanifu na ifikapo
Juni mwakani uchimbaji utaanza rasmi.
"Nia
yetu ni hadi kufikia Disemba mwakani tuwe na gati kuanzia sifuri hadi
namba tatu na upanuzi wa lango uwe
umekamilika ili tuweze kupokea meli za
kimataifa zenye kina cha mita 15 na uwezo wa kubeba hadi makasha 6000 kutoka
meli za sasa zinazoweza kubeba makasha 2500 tu," alisema Kakoko.
Aliongeza,
"Watu wa meli wajiandae hapa meli zitakuwa zinapishana kama daladala
zinavyopishana, bandari hii ipo kwenye eneo ambalo Mungu amelibariki kijografia
katika ukanda huu kuanzia Misri hadi Afrika Kusini na kwa sasa biashara ya
dunia imehamia upande wa Mashariki kutoka Magharibi.
"Hivyo
miaka mitatu ijayo tuna uhakika wa kurudisha ule utukufu wa bandari ya Dar es
Salaam," alisisitiza.
Akifafanua
zaidi kuhusu mradi huo Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi TPA, Charles
Ogale, alisema mradi huo unahusisha
uongezaji wa kina cha kutoka mita sita hadi mita 12.9 kutoka usawa wa bahari
baada ya maji kupwa, upana wa mita 34 na itakuwa na urefu wa mita 320 pamoja na
ujenzi wa yadi yenye ukubwa wa mita za mraba 69,000.
Alisema
mradi mzima wa upanuzi wa gati ya magari ambayo ni 'zero berth' hadi gati namba
saba ulioanza Juni 2017 unatarajiwa kukamilika Juni 29 2020.
"Upanuzi
huu umeiongezea gati uwezo wa kubeba meli kubwa zaidi pasipo kupata misukosuko
yeyote ," amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdediti Kakoko, akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Fredy Lihundi, akifafanua jambo
Wakandarasi wanaofanya upanuzi katika Bandari ya Dar es Salaam, wakijadili jambo katika mradi huo na viongozi wa TPA.
Mtambo wa kuchimba kina cha Bahari ukimwaga mchanga nje ya bahari katika Bandari ya Dar es Salaam,
No comments:
Post a Comment