DAR ES SALAAM, TANZANIA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura na wanaoishi kwenye kata Sita za Tanzania Bara, kujitokeza kwa wingi
kupiga kura siku ya Jumapili Desemba 2 mwaka huu ili kuwachagua viongozi wanaowataka
wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.
Wito huo umetolewa na
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage wakati akisoma
risala ya uchaguzi mdogo wa Udiwani unaohusisha kata za Miteja,
Kivinje au Sigino , Somanga na Mitole katika Halmashauri ya Kilwa, kata ya Muhinda katika Halmashauri ya Wilaya ya
Buhigwe na Kata ya Nkoanekoli katika
Halmashauri ya wilaya ya Meru.
“Wapiga
Kura wapatao 31,818 wanatarajiwa kupiga Kura kuwachagua Madiwani katika Kata 6
za Tanzania Bara na uchaguzi huo utafanyika katika Vituo 91 vya Kupigia Kura
ambako ndipo Wapiga kura walijiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa
Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015.
Aliwataka kwenda kupiga
kura bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi kwani chini ya Kanuni ya 3.1 (b) ya
Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Serikali
imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani na utulivu
katika kipindi chote cha Uchaguzi.
Mbali na wito huo, Jaji
Kaijage aliwataka wananchi, vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi
kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu
vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.
Jaji Kaijage alivisisitiza
vyama vya siasa kufanya mikutano ya
kampeni inatakiwa kufikia mwisho leo Jumamosi saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni na
baada ya muda huo, vyama, wagombea na mashabiki waache kufanya kampeni za aina
yoyote, kama vile kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni, vipeperushi,
bendera, mavazi na vitu vingine visivyokubalika katika siku ya Uchaguzi.
“Aidha, wananchi waheshimu
Sheria za Nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza
matokeo. Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa Sheria na
Taratibu za Uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa
utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.”, alisema Jaji Kaijage na kuongeza
kuwa:
“Vivyo hivyo, Viongozi wa
Vyama vya Siasa, Wagombea au wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na
vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu katika vituo vya Kupigia,
Kuhesabia na Kujumlishia Kura.”
Jaji Kaijage aliwataka
wapiga kura kuondoka kwenye maeneo ya kituo cha kupigia kura mara baada ya
kupiga kura na kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya
kupigia kura kwani vyama vya siasa vimeweka mawakala vituoni ambao watalinda
maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
Mwenyekiti huyo wa NEC,
alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, wananchi na watendaji wa uchaguzi kwa
ujumla kuzingatia na kuheshimu matakwa na masharti ya Sheria za Uchaguzi,
Sheria za Nchi, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi wakati wa Upigaji Kura, Kuhesabu,
Kujumlisha Kura, na Kutangaza matokeo.
Alisema upigaji kura
utafanyika kuanzia saa moja kamili asubuhi na kumalizika saa kumi kamili jioni
katika vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kwamba
watakaokuwepo kwenye mstari kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia saa kumi
kamili jioni wataruhusiwa kupiga kura.
Hata hivyo, alibainisha
kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu waliomo kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura kwenye Kata husika na wana kadi ya mpiga kura na wale waliopoteza
kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa wataruhusiwa kupiga kura
kutumia Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia
kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa sharti kuwa
majina yaliyomo kwenye vitambulisho hivyo yafanane na yale yaliyomo kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Ni wajibu wa vyama vya
siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi kuweka mawakala katika vituo vyote vya
Kupigia na Kujumlishia Kura kwa utaratibu ambao tulikubaliana na umekuwa
ukitumika katika chaguzi za hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Tume na Vyama
vya Siasa tarehe 10/07/2018 uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano
wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam, na maelekezo kuhusiana na utaratibu
huo kutumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi.”, alikumbusha Jaji Kaijage.
Hata hivyo, alisema
mawakala hao wanaruhusiwa kuwepo katika Vituo vya Kupigia Kura na wanatakiwa
kufuata na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika
kipindi chote cha kupiga, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
No comments:
Post a Comment