WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezinduaMkakati
wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2018/19 - 2022/23 ambao unatarajia
kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na
asilimia 85 ifikapo mwaka 2023.
Matokeo mengine yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua
kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia 5
ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2 ifikapo mwaka 2030.
Waziri
Mkuu amezindua mkakati huo leo (Jumamosi, Desemba 1, 2018) kwenye
kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika Kitaifa
jijini Dodoma na kusema kuwa matayarisho yake yamezingatia matokeo ya
mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 –
2017/18.
Amesema
mbali na matokeo hayo pia mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo
vinavyohusiana na ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na
asilimia 70 ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi
ifikapo 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema mkakati huo umewianisha na kupanga programu
mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa
kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa uKIMWI (PEPFAR).
“Pia
Mfuko wa Dunia wa kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Globa Fund)
na jitihada nyingine za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi
mbalimbali na ili kupata matokeo mazuri tunapaswa kuimarisha mawasiliano
na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kufuata na kutekeleza
vipaumbele vilivyoainishwa.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema maadhimisho
hayo husaidia kubaini changamoto, mafanikio na hivyo, kuja na mikakati
ya kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI. “Siku hii hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano ya UKIMWI kwenye jamii zetu.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu faida za kampeni ya FURAHA
YANGU aliyoizindua mwezi Juni mwaka huu, ambapo aliagiza mikoa yote
kufanya uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye ngazi za mikoa na hata wilaya.
Amsematakwimu
zinaonesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU katika
mikoa yote nchini jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU,
wakiwemo wanawake 136,389 na wanaume 125,725.
“Natoa
wito kwa Mikoa na Wilaya zote kuwa kampeni hii iwe endelevu. Viongozi
katika ngazi mbalimbali tuungane kwenye uhamasishaji wa jambo hili kwani
vita dhidi ya VVU na UKIMWI inahitaji dhamira ya dhati na tafakuri ya
kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.”
Waziri
Mkuu amewahakikishia kuwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za
upimaji wa Virusi Vya UKIMWI, kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi na kupiga vita
unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora wakipita kwa maandamano mbele ya Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani
Kitaifa, kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini Dodoma, Desemba 1, 2018.
(Picha zote Ofisi ya Waziri Mkuu).
Wananchi wakiingia kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini Dodoma
kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa, Desemba
1, 2018. Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika
Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini
Dodoma, Desemba 1, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa
Kudhibiti Ukimwi Tanzania (2018/19 – 2022/23) katika Maadhimisho ya Siku
ya Ukimwi Duniani Kitaifa, kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini Dodoma,
Desemba 1, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na Kulia
ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dkt. Faustine Ndugulile na Kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Kitabu cha Mkakati wa
Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (2018/19 – 2022/23) baada ya
kuzindua Mkakati huo katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani
Kitaifa, kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini Dodoma, Desemba 1,
2018. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na Kulia ni Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine
Ndugulile.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Kitabu cha Mkakati wa
Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (2018/19 – 2022/23) Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Nchini, Alvaro Rodriguez baada ya
kuzindua Mkakati huo katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani
Kitaifa, kwenye Kiwanja cha Jamhuri jijini Dodoma, Desemba 1, 2018.
Watatu kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na Kulia ni Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine
Ndugulile na Kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko.
No comments:
Post a Comment