WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB)
ihakikishe inabadilisha mfumo wake ili iweze kuharakisha malipo kwa
wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatano, 16 Januari, 2019) wakati akizungumza na Wakuu
wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TADB
kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing)
kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.
Wakuu wa mikoa hiyo mitatu walikuwa kwenye mikoa yao na Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alikuwa Dar es Salaam.
“Hakikisha
mnaharakisha malipo ya wakulima lakini pia suala la uhakiki linabaki
palepale ili tuwalipe wakulima wanaostahili,” amemweleza Mkurugenzi Mkuu
wa TADB, Bw. Japhet Justine.
Waziri
Mkuu amesema Serikali bado inapokea malalamiko kutoka kwa wakulima
kuhusu suala la malipo ya korosho kwani kwa kawaida malipo ya mkupuo
yote huwa yamekamilishwa ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.
“Matarajio
yetu yalikuwa ni kuvuna tani 245,000 au zaidi kidogo lakini umesema
hadi sasa korosho zilizo kwenye maghala ni tani 206,000 maana yake
takriban tani 40,000 ziko AMCOS au majumbani kwa wakulima. Na ambazo
mmezilipia hadi sasa ni tani 92,000 na pointi zake. Tuko chini ya nusu.”
“Hili
zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe
16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili
tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani! Tunapata lawama kutoka kwa
wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo; na haya siyo malengo
ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali.”
Waziri
Mkuu alihoji ni kwa nini benki hiyo haishirikiani na vyama vikuu
(unions) au vyama vya msingi (AMCOS) ili kubaini idadi halisi ya
wakulima na idadi kamili ya kiasi walichovuna kwa sababu kila AMCOS ina
wanachama wake wanaojulikana.
“Zao
la korosho lina mfumo wa ushirika. AMCOS ziko kwenye ngazi ya vijiji na
unaweza kukuta AMCOS moja ina wanachama zaidi ya 200, sasa bila kupitia
kwenye hizi AMCOS unawezaje kujua kila mkulima amevuna kilo ngapi na
anadai kiasi gani kwa kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee?
“Kuna
Wilaya zina AMCOS zaidi ya 50. Ni kwa nini msitumie mfumo huo lakini
mkawatenga kwenye makundi mawili yaani wakulima wenye chini ya kilo
1,500 au zaidi ya 1,500 ili muweze kufanyia uhakiki kwa urahisi?”
aliluliza.
Ameitaka
benki hiyo izishirikishe AMCOS na UNIONS pindi malipo yanapofanyika ili
nao wajue ni wanachama wao gani ambao wameshalipwa. “Mfumo unaotumika
sasa unapeleka malipo moja kwa moja kwenye akaunti ya mtu binafsi, kwa
hiyo AMCOS wanakuwa hawana taarifa, na wao pia wanachangia kushiriki
kutoa malalamiko.”
Waziri
Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa mikoa hiyo wahuishe
taarifa zao na wamtumie ili aweze kuzitumia kuratibu zoezi zima.
“Mniletee taarifa zenu mkionesha ni kiasi cha korosho mlitarajia
kuzalisha; mmeshakusanya kilo ngapi hadi sasa ambazo ziko kwenye
maghala; kama malipo yameanza, ni wakulima wangapi wameshalipwa; na
fedha kiasi kila mkoa umeshapokea hadi sasa,” amesisitiza.
“Nimeongea
na wakurugenzi wa CRDB na NMB na kuwasisitiza kuwa suala la miamala ya
malipo ya korosho lifanywe mchana na usiku ili malipo yakamilike kabla
ya Januari mwishoni,” amesema.
Kwa upande wao, wakielezea
changamoto wanazokabiliana nazo, wakuu hao wa mikoa walisema kuwa suala
kubwa ni ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, baadhi ya AMCOS na vyama
vya msingi kulipwa mara nyingi zaidi ya vyama vingine, miamala ya
malipo ya wakulima kukataliwa na Benki na hali ya kutoaminiana baina ya
timu ya uhakiki na watendaji wa wilaya na mikoa ambao ni wajumbe wa
Kamati za Ulinzi na Usalama.
Mapema, Mkurugenzi
Mkuu wa TADB, alisema fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi
sasa ni sh. bilioni 306 kwa wakulima zaidi ya 156,000. “Korosho
zilizolipwa hadi sasa ni tani elfu 92.7 ambazo ni wastani wa asilimia
44,” alisema.
Hata
hivyo, Bw. Justine alisema zaidi sh. bilioni 11 zimekwama kulipwa kwani
taarifa za kibenki zinaonyesha kuna matatizo hasa kwenye majina.
“Majina
ya waliopeleka mzigo, yanatofautiana na majina ya akaunti za benki.
Majina yaliyokataliwa na mfumo wa kibenki yatabandikwa kwenye vyama vya
msingi ili wakulima wakarekebishe taarifa zao,” alisema.
Alisema takriban sh. bilioni 15 zimelipwa wa watoa huduma ambao ni wasafirishaji, wapagazi na wenye maghala.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
JUMATANO, JANUARI 16, 2019.
No comments:
Post a Comment