Picha tofauti zikimuonyesha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho Soka Tanzania (TFF), Hamidu Mbwezeleni enzi za uhai wake.
NA MAKUBURI ALLY
RAIS wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia amepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha
aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo, Hamidu Mbwezeleni
kilichotokea jana.
Kwa mujibu wa Ofisa
habari wa TFF, Clifford Ndimbo, Rais Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi
kwa familia ya Mbwezeleni, ndugu jamaa na marafiki wa soka hapa nchini.
Alisema kipindi cha
uhai wake, Mbwezeleni alikuwa mwanamichezo mzuri ambaye alishiriki katika
shughuli mbalimbali za soka.
“Kwa niaba ya TFF
natoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wanafamilia wa soka kwa msiba huu
mkubwa,” alisema Karia.
Alisema Mbwezeleni
alikuwa ni mwenye weledi katika shughuli mbalimbali alizokuwa akifanya ambazo alizifanya kwa uhodari.
Katika kipindi chote
alichokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF alifanya kwa moyo wake wote
wa kuutumikia mpira wa Tanzania.
Rais Karia amewaomba
wafiwa kuwa na subira katika kipindi chote cha msiba na TFF iko karibu nao.
Mbwezeleni atakumbukwa
kwa kuwafungia maisha kutojihusisha na shughuli za Soka Makamu wa Rais wa TFF,
Michael Wambura kutokana na kupokea fedha zisizo halali kiasi cha Shilingi
milioni 84, kugushi nyaraka za malipo, na kula njama kulipwa fedha, adhabu
ilianza Machi 15, 2018.
Agosti 27, 2018 Mjumbe
wa kanda ya Shinyanga, Mbasha Matutu alifungiwa maisha na kamati ya Mbwezeleni,
Matutu alifungiwa kwa makosa matatu ya
kushindwa kutekeleza majukumu yake, ubadhirifu, kughushi na kuiba kinyume na
kanuni za Maadili na Ligi Kuu.
Ambako kabla, Mjumbe
wa Kanda ya Mtwara na Lindi, Dunstun Mkundi pia alifungiwa maisha kutojihusisha
na soka kwa makosa ya kughushi.
Novemba 5, 2018,
aliyekuwa Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatus Kuuli naye
alifungiwa maisha kutojihusisha na soka na Kamati ya Maadili kwa makosa ya
kusambaza taarifa alizotumiwa na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao.
Kama hiyo haitoshi,
Kamati ya maadili iliwafungia maisha, viongozi wa Chama cha Soka Arusha (ARFA),
Mwenyekiti Peter Temu, Katibu msaidizi Nassoro Mwarizo.
Wengine ni mweka
hazina wa ARFA, Omar Nyambuka na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Chama hicho
Hamis Issah alifungiwa miaka mitano.
Pia Kamati ya
Mbwezeleni ilimfungia mwaka mmoja Meneja wa timu hiyo, Robert Richard kwa
makosa ya maadili.
No comments:
Post a Comment