HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2019

KAMISHNA WA FIU; ATOA RAI KWA SEKTA YA BIMA NA MASOKO YA MITAJI JUU YA UTAKASISHAJI FEDHA

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
 
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) imeendesha warsha kuhusu udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa wadau wa sekta ya bima (insurance sector) na masoko ya mitaji na dhamana(capital markets and securities sector) kwa lengo la kuendelea kuwakumbusha wadau kuhusu umuhimu wa kuendelea kutekeleza wajibu wao na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na uhalifu wa kifedha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili juu ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi inayofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Ndugu Onesmo H. Makombe anasema warsha hii muhimu ni muendelezo wa warsha kuhusu udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi katika sekta ya benki.

Alieleza kuwa tatizo la utakasishaji wa fedha haramu ni tatizo kubwa ulimwenguni kote na katika jamii kwasababu ya kuwepo kwa vitendo mbalimbali vya uhalifu vinavyowapatia wahalifu pato haramu. Uhalifu huo ni pamoja na ukwepaji kodi, biashara haramu ya dawa za kulevya, biashara haramu ya watu, biashara haramu ya silaha, rushwa, kughushi, ujangili, uharamia, uvunaji haramu wa magogo, uuzaji wa bidhaa bandia, ujambazi na uporaji.

“pamoja na utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi, kuendelea kujenga na kuimarisha mifumo ya udhibiti katika taasisi ili kuzuia uwezekano wa sekta za bima na masoko ya mitaji na dhamana kutumika na wahalifu kama vyombo vya kutakasisha fedha haramu na kufadhili vitendo vya ugaidi. Kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti katika sekta hizi kutasaidia kulinda mfumo wa fedha wa nchi yetu ili usitumiwe na wahalifu na watu wasio waaminifu”.

Aidha, aliainisha madhara ya utakasishaji wa fedha haramu kuwa ni ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama. Madhara hayo pamoja na uhalifu kuendelea kushamiri kwa uhalifu na wahalifu kujiimarisha; wahalifu kuwa na nguvu kiuchumi; kuhatarisha utawala wa sheria na usalama (threaten peace, stability and rule of law) kwani uhalifu unaposhamiri na makundi ya uhalifu yanapojiimarisha hupata nguvu na kujaribu kudhibiti kushindana na vyombo vya dola; kuharibu ushindani (ruin competitiveness) wa kibiashara katika uchumi kutokana na wahalifu kuwa na mitaji inayotokana na fedha haramu, wafanyabiashara halali hushindwa kuhimili ushindani; kushusha hadhi ya nchi kimataifa (erosion of country’s integrity) na kusababisha nchi kutonufaika na mfumo wa fedha wa kimataifa.

Aidha na kushusha imani ya wawekezaji na kusababisha uwekezaji kupungua na wawekezaji wapya kutotaka kuwekeza kutokana na kushamiri kwa uhalifu, wawekezaji huwa na hofu kuwa mitaji na mali zao havitakuwa salama; imani ya washirika wa maendeleo na jumuiya ya kimataifa hupungua na nchi huathirika kiuchumi; kushuka kwa hadhi ya taasisi za fedha na mfumo mzima wa fedha; na nchi kushindwa kufikia malengo ya maendeleo kwani rasilimali huwa mikononi mwa wahalifu wachache badala ya kutumika kutekeleza ajenda pana ya maendeleo ya nchi.

Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu amewaasa na kuwakumbusha washiriki wa warsha hiyo kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutekeleza wajibu wao wa kisheria kwa uadilifu na uaminifu ili kuendelea kusaidia katika kubaini wahalifu wanaoweza kutumia mfumo wa fedha wa nchi kutakasisha fedha haramu na kufadhili vitendo vya kigaidi na kuhatarisha usalama wa nchi.
Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Ndugu Onesmo H. Makombe Akitoa neno wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili juu ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi inayofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam.Kamishna Msaidizi Huduma za Kompyuta kitengo cha kudhibiti fedha haramu(FIU),Gilbert Nyombi akitoa mada juu ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi inayofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania,
Mmoja ya Washiriki wa Warsha hiyo Floransia Mrema akichangia jambo wakati wa Warsha hiyo.
Washiriki wa Warsha hiyo wakimsikiliza kamishna wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili juu ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi inayofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania,

Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Ndugu Onesmo H. Makombe, akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya Bima na Masoko ya Mitaji ya Dhamana, katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages