NA JOHN MARWA
NI kama vile filamu! Mchakato wa uchaguzi wa kuziba nafasi zilizo wazi ndani ya Klabu ya Yanga umezidi kuchukua sura mpya baada ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliofungua kesi kuupinga kubainika kuwa si wanachama.
Kutokana na hilo, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema sasa mchakato huo unaendelea unaendelea baada ya kutupiliwa mbali mashauri ya kesi zilizofikishwa Mahakamani kupinga uchaguzi huo hivi karibuni.
Uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Januari 13 mwaka huu, lakini ulisitishwa kutokana na baadhi ya waliodhaniwa kuwa ni wananchama wa klabu hiyo, kufungua kesi ndani ya mikoa mitatu kuupinga.
Januari 11 mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela, alitoa taarifa ya kusitishwa kufanyika kwa uchaguzi huo kutokana na wanachama hao kufungua kesi Mahakamani, wakipinga uhalali wa Wanachama wa kadi za CRDB na Posta.
Pili, kukataliwa majina ya baadhi ya wanachama kuingizwa kwenye kitabu cha uchaguzi na tatu sintofahamu ya nafasi ya Mwenyekiti, kiasi cha wagombea wengine kushindwa kujitokeza kugombea katika uchaguzi huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mchungahela, alisema baada kukaa na kupitia taarifa za Wanachama waliopeleka kesi mahakamani, walibaini kuwa sio hai.
“Wanachama waliopeleka kesi Mahakamani ni mmoja tu ndiye mwanachama hai, wakati wawili sio wanachama hai, jambo ambalo linawanyima sifa ya kusimamisha uchaguzi.
“Katiba ya Yanga SC, TFF, CAF na FIFA, haziruhusu wanachama kupeleka kesi mahakamani, bali kesi hizi zinahitajika kumalizwa na TFF, kwa hiyo wamekiuka katiba,”alisema Mchungahela.
Mchungahela, alisema waliongea na wanachama hao waweze kufuta kesi hizo mahakamani na wamekubaliana kufanya hivyo.
Kuhusu kadi zitakazotumika katika uchaguzi baada ya mwanachama mmoja halali aliyesalia kuhitaji kutumika kwa kadi za zamani, licha ya awali kutangazwa kuwa wanachama wote hai wanaruhusiwa kupiga kura, alisema watalitolea ufafanuzi kabla ya uchaguzi huo.
“Hivyo basi, mchakato wa uchaguzi unaendelea na ndani ya siku saba kuanzia jana tutawatangazia tarehe ya kufanyika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ndani ya klabu ya Yanga,” alisema.
Pia, aliwataka wanachama wa Yanga kuanzia kwa Baraza la Wadhamini, kuwa na imani kwani mchakato huo umefika ukingoni na muda si mrefu watapata viongozi kwa maslahi mapana ya soka na maendeleo ya klabu.
No comments:
Post a Comment