Imani
za kishirikina, visasi vyatajwa
Na
Mwandishi Wetu
Hali ya majonzi, vilio
na simanzi ilitawala wakati wa mazishi ya miili ya watoto watatu wa familia moja
waliouawa kikatili ikiwa takribani mwezi mmoja sasa tangu matukio ya kupotea na kuuawa kwa watoto katika
Wilaya ya Njombe.
Akizungumza katika
mazishi ya watoto hao watatu;Godliver Mwenda(11), Gasper Nziku(8) na Geribet
Nziku(5), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni
amesema Serikali inalaani mauaji hayo na imejipanga kuhakikisha inadhibiti na
kutokomeza mtandao huo unaojihusisha na mauaji hayo ya kikatili kwa watoto
“Tukio hili halitopita
bure bure na tunataka iwe fundisho kwa watu wengine wote wenye roho za kinyama
waliotekeleza mauaji haya na tayari baadhi ya watuhumiwa wa mauaji haya tayari
washakamatwa kwa kupitia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likwemo jeshi la
polisi,” alisema Masauni
“….nataka nitoe ujumbe
huu kwa nchi nzima kwamba mtu yoyote ambae
anajishughulisha na mauaji dhidi ya binadamu ikiwemo watoto wadogo kama
hawa tunamuhakikishia tutamkamata na serikali haitolala katika hili” aliongeza
Masauni
Akizungumza wakati wa
mazishi hayo Baba wa marehemu hao,Danford Nziku ameiomba Serikali kuimarisha
ulinzi maeneo mbalimbali katika kijiji hicho huku akisisitiza kutafutwa kwa
watuhumiwa waliohusika na mauaji ya watoto wake
“Watoto wangu
wameondoka wakiwa bado na umri mdogo sana, ndoto zao sasa zimezimwa ghafla
baada ya kufanyiwa ukatili,na wao sio wa kwanza kufanyiwa matukio hayo ndani ya
mwezi huu, naiomba serikali yangu kuimalisha ulinzi katika maeneo haya,sasa
naishi kwa hofu hapa nyumbani na mke wangu” alisema Baba wa marehemu hao.
Akizungumza kwa sharti
la kutotajwa jina lake mkazi wa Kijiji cha Ikando wilayani Njombe, amesema
matukio hayo yametokea sana kipindi cha nyuma huku akiiomba serikali kupiga vita ramli
chonganishi, kupitia uhalali wa waganga wa kienyeji waliopo wilayani hapo.
“Vifo hivi
vinasikitisha nadhani serikali iandae utaratibu wa kuhakiki hawa wataalamu wetu
wa kienyeji, wamekua chanzo cha malumbano mengi hapa kijijini, watu wamekua
wakituhumiana mambo ya uchawi hali inayopelekea kuwepo kwa visasi kati yao
ambavyo hupelekea vifo kama hivi,” alisema mwananchi huyo
Akizungumza juu ya
mauaji hayo Kaimu Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Kibena, Barnabas Baraka amesema vifo vya watoto hao vimetokana na
kushambuliwa na vitu vizito na vyenye kali maeneo ya kichwani huku mmoja kati
ya maiti hizo akiwa amekatwa sikio la kulia.
Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi waliohudhuria
mazishi ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando
Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, ambapo aliahidi Serikali kukomesha mauaji
hayo.Picha
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiweka mchanga katika moja ya
makaburi ya watoto watatu wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha
Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe.
Moja ya jeneza
lililobeba mwili wa mmoja wa watoto wa familia moja waliouawa kikatili katika kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe, likiingizwa
kaburini wakati wa mazishi hayo.
Ndugu wa familia
iliyopoteza watoto watatu wakiweka kaburini nguo za mmoja wa watoto hao ikiwa
ni utekelezaji wa mila na desturi ambapo marehemu huzikwa na nguo zake zote.Mazishi
hayo yamefanyika katika Kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani Njombe.
Waombolezaji wakiwa
wamebeba majeneza ya watoto watatu; Godliver
Mwenda, Gasper Nziku na Geribet Nziku wa familia moja waliouawa kikatili katika
kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa, wilayani
Njombe.
No comments:
Post a Comment