HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 26, 2019

RAIS MAGUFULI AMLILIA RUGE MUTAHABA

Ruge Mutahaba enzi za uhai wake.

NA MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA mmoja wa Wakurugenzi na wawaanzilishi wa Kituo cha Redio na TV Clouds Media, Ruge Mutahaba amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo chake  zimesema kuwa Ruge alifariki dunia leo majira ya saa moja usiku.
Kutokana na kifo hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akieleza kwamba amesikitishwa na ameguswa sana na kifo hicho.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitakumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu amweke Mahali Pema Peponi Amina.
Ruge ambaye wakati akiugua Rais Magufuli alichanga shilingi milioni 50 kwa ajili ya matibabu yake ambayo taarifa zinasema yalikuwa na gharama kubwa.
Kutokana na gharama hizo zinazokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 20 kwa siku, kituo cha redio na TV Clouds  kiliamua kutoa matangazo ya kuwataka wananchi kuchangia gharama za matibabu yake.
Ruge pamoja na mambo mengine atakumbukwa sana kwa mchango wake kwa wasanii mbalimbali ambao leo wamekuwa nyota na wamepata mafanikio mengi ndani na nje ya nchi.
Lakini pia amekuwa mbunifu wa kuanzisha fursa za ujasiriamali kwa vijana ambapo kila mwaka kupitia kituo chake cha redio na tv alikuwa akizunguka mikoa yote kutoa semina na mbinu za ujasiriamali na namna ya kujikomboa kiuchumi. Mungu amweke Mahali Pema Peponi, Amina.

No comments:

Post a Comment

Pages