Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama , akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.
Baadhi ya waandishi wa habari.
Na Mwandishi Wetu
WAKATI wadau na wapenzi wa muziki wa injili jijini
Dar es Salaam wakisubiri kwa hamu kuona ni sura zipi za waimbaji watakuwemo
katika Tamasha la Pasaka la mwaka huu, Kamati ya Maandalizi imetangaza Uwanja
utakaotumiwa siku hiyo.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama alisema kwamba kwa jiji
la Dar es Salaam, uhondo wa tukio hilo la kimataifa utafanyika katika Uwanja wa
Kijitonyama TCCL Posta, wilayani Kinondoni.
Msama
alisema kuwa, hadi sasa maandalizi yamezidi kushika kasi kwani tayari
wameshakamilisha mazungumzo na mmoja wa waimbaji mahiri wa kimataifa ambaye kwa
umaarufu wake, ndiye atabeba uzito wa tukio hilo la mwaka huu.
“Tunashukuru
Mungu, maandalizi yanakwenda vizuri sana kwani hadi sasa tumeshakamilisha
mazungumzo na mwimbaji mmoja wa kimataifa ambaye ndiye atabeba uzito wenyewe wa
tamasha la mwaka huu,” alisema Msama.
Alisema jina
la mwimbaji huyo litawekwa bayana baadaye, lakini akidokeza kuwa ni mwimbaji
mahiri ambaye kila mdau wa nyimbo za injili, atamkubali kutokana na uwezo na
kipaji chake.
Kuhusu
Uwanja wa Kijitonyama, Msama alisema kuwa Kamati yake imefanya utafiti wa kina
kabla ya kufikia uamuzi huo, ikiwemo ukubwa wa eneo, usalama pamoja na wepesi
wausafiri wa kwenda na kurudi.
“Tumetafakari
sana ni uwanja gani unafaa kwa ajili ya kufanyia tukio hili la kimataifa.
Tukaona ni Viwanja vya Kijitonyama kwa sababu ni rahisi kufika na usalama wake
kwa watu na mali zao ni mkubwa mno,” alisema Msama.
Msama
alisema baada ya tukio hilo kutumbuiza wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili
wa Dar es Salaam, litahamia katika
mingine 10, likianzia jijini Dodoma, Singida, Simiyu na Mwanza.
Alisema
mikoa mingine zaidi itakayofikiwa na Tamasha hilo, itajulikana baadaye kwa
kadiri maandalizi yanavyoendelea kwani lengo ni kuhakikisha uhondo huo unafika mikoa
mingi zaidi ili ujumbe wa Neno la Mungu uweze kuwafikia wengi.
Alisema
mbali ya tamasha hilo kutumika kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa neno la Mungu
kwa njia ya kuburudisha, pia sehemu ya mapato hutumika kufariji wenye mahitaji
maalumu kama walemavu, wajane na yatima katika jamii.
Msama
alisema kwa mwaka huu, Tamasha hilo ambalo linahimiza umuhimu wa hali ya amani
na upendo katika taifa, linaangaza juhudi za serikali katika miradi ya
maendeleo iliyofanyika na inayoendelea kufanyika kwa kasi kote nchini.
Alisema
Tamasha hilo limejitosa kuhimiza amani na upendo katika taifa kwa kutambua,
vitu hivyo viwili ndio msingi wa watu na taifa kupiga hatua katika nyanja zote
za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Msama kwa
mutambua hiyo, ndio maana anawasihi wadau na wapenzi wa muziki wa injili, kukaa
mkao wa kupokea uhondo wa Tamasha hilo ambalo litabeba uzito mkubwa wa waimbaji
mahiri wa kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment