Benny Mwaipaja, WFM, Dar
es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati
kukamilisha mradi mkubwa wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ambapo tayari
kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 2 kimetolewa mpaka sasa kwa ajili ya
ujenzi huo.
Dkt. Kijaji ametoa kauli
hiyo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli hiyo kutoka Dar
es Salaam hadi eneo la Soga, umbali wa kilometa 53, na kujionea maendeleo makubwa
ya ujenzi wa reli hiyo.
Ameelezea kuridhishwa
kwake na kasi ya ujenzi wake na kumpongeza mkandarasi anaye jenga reli hiyo,
Kampuni ya Yapi Merkezi, kwa kutekeleza ujenzi huo kwa viwango vya hali ya juu
ambapo ameelezwa kuwa, treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro
inatarajia kuanza safari zake Mwezi Novemba mwaka huu kama kila kitu kitakwenda
kama kilivyopangwa.
"Ninampongeza sana
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake kubwa na kuamua kwa dhati
kutekeleza mradi huu mkubwa na miradi mingine, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme
kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambayo kukamilika kwake
kutachochea uchumi wa viwanda" alisema Dkt. Kijaji
"Tunakwenda
kwenye Tanzania ya viwanda, tutakuwa na viwanda kila mahali, tumeanza
ujenzi wa mradi wa umeme wa megawat 2,115, viwanda vitazalisha bidhaa
ambazo zitahitaji miundombinu ya usafirishaji, reli hii itatumika na
tunatarajia ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa ni nchi yenye kipato
cha kati" aliongeza Dkt. Kijaji
Kwa upande wake, Meneja wa
Mradi wa Ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi
Machibya Masanja, amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo umekamilika kwa asilimia 42.
"Mradi wetu unaenda
vizuri na kwa wakati, zoezi la ujenzi na utandikaji reli tumeanza katika Jijini
la Dar es Salaam umeanza na unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa daraja hilo umekamilika
kwa asilimia 55 na utandikaji wa reli katika Jiji hili utafikia kilometa 10
mwishoni mwa mwezi Februari" alifafanua Mhandisi Masanja.
na nguvu kubwa imeelekezwa
katika ujenzi wa tuta na madaraja, zezi ambalo limefikia asilimia 55 hivi
sasa" alifafanua Mhandisi Masanja
Ujenzi wa Reli kwa Kiwango
cha Kimataifa kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma hadi Mwanza, na baadae
kuunganisha mtandao wake na nchi jirani za Kongo, Uganda, Burundi na Rwanda,
unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 7.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezungumza na wakazi wa
eneo la Guluka Kwalala, Gongo la Mboto, waliokuwa wakiendelea na taratibu zao
za kulipwa fidia ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaletea
maendeleo.
Baadhi ya wakazi hao,
pamoja na kuiomba Wizara ya Ardhi na Makazi iwasaidie kupata viwanja kwa ajili
ya kujenga makazi yao baada ya kulipwa fidia kupisha ujenzi wa mradi huo wa
Reli ya Kisasa, wamempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kusimamia ustawi na maendeleo ya nchi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.
No comments:
Post a Comment