Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) amemuandikia barua
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu kuwa
Jimbo la Arumeru Mashariki linaloongozwa na Mheshimiwa Joshua Nassari
aliyedhaminiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lipo
wazi kutokana na Mbunge huyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa Mbunge.
Mheshimiwa Nassari amepoteza sifa za kuwa Mbunge kutokana na kitendo chake cha kutohudhulia vikao vya Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo. Mikutano hiyo ni Mkutano wa Kumi na Mbili wa tarehe 4 -14 Septemba 2018, Mkutano wa Kumi na Tatu wa tarehe 6- 16 Novemba 2018 na Mkutano wa Kumi na Nne wa tarehe 29 Januari – 9 Februari 2019.
Uamuzi huo wa Mheshimiwa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1)(c). Ibara hiyo inaeleza kuwa “Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge Mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika”
Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika Kanuni ya 146 (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo ya Januari 2016. Kanuni hiyo inaeleza kuwa “Kuhudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake ni wajibu wa kwanza wa Mbunge, Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza Ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi”
Kufuatia barua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki.
Imetolewa na:- Kitengo Cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge.
No comments:
Post a Comment