NA JOHN MARWA
WANATOKAJE! ndivyo
unaweza kusema kuelekea mchezo wa leo mjini Morogoro Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara TPL Simba SC wakiwakabili
vilivyo wabishi wa jijini Mwanza, Mbao FC.
Simba wanashuka kwenye
mtanange huo wakiwa na hasira za kulipa kisasi cha kuchapika bao 1-0 pambano la
ungwe ya kwanza lililopigwa Septemba 20, 2018 Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza.
Wakitoka kupata
mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika CAF CL na kuwasasambua Ruvu
Shooting mabao 2-0, wanaingia fulu mzuka kuwakabili Mbao ambao wamewatia doa
msimu huu ikiwa timu pekee ilkiyoifunga Simba hadi sasa.
Simba wanahitaji
ushindi kuendeleza mapambano ya kutetea ubingwa wao, wakiwa wameshacheza
michezo 21 pointi 54 nafasi ya tatu mechi 7 nyuma ya vinara wa TPL Yanga wenye
pointi 67 mechi 28.
Wabishi wa Mbao
wanashuka kwenye mtanange wa leo wakishika nafasi ya 15 kwenye msimamo na
pointi 36 za michezo 30.
Mbao FC wamefanikiwa kushinda
mechi tisa sare tisa huku wakipoteza 12, wamefunga mabao 19 na kuruhusu 29,
wastani wa kufumania nyavu ni 0.63 katika kila mchezo na wa kufungwa ni 0.96, sawa
na bao moja kila mechi.
Wakati huo kikosi cha Mbelgiji
Patrick Aussems badaa ya kushuka dimbani mara 21, kimeshinda mapambano 17 sare tatu
na kupoteza dhidi ya wabishi hao.
Hadi sasa Simba
wametikisa nyavu za wapinzani wao mara 45, huku wakiwa wameruhusu mabao machache
zaidi hadi sasa yakiwa ni saba ya
kufungwa.
Takwimu zinaonyesha
Simba kuwa na safu imara zaidi sambamba na safu ya ushambuliaji ikiwa imetupia
mabao hayo 45 michezo michache zaidi ya wapinzania wake wa karibu Yanga na Azam
wakiwa na mabao 46 ya kufunga ndani ya michezo 28.
Wastani wa Simba kutikisa
nyavu katika kila mchezo ni mabao 2.14 huku wakiruhusu lango lao kutikiswa ni
0.33 kwa mtanange.
Katika michezo mitano
iliyopita kunako TPL Simba wamepata matokeo kwa asilimia 100, wakishinda
michoze yote huku Mbao ni asilimia 80,
wakishinda mmoja na kupoteza minne.
Katika michezo 15
waliyocheza ugenini Mbao hadi sasa wameshinda mechi mbili sare tano na kupoteza
minane, huku Simba ni michezo 10 wakishinda nane sare moja na kupoteza moja.
Wakati katika michezo
ya nyumbani Mbao wamecheza michezo 15 wakipata matokeo mechi saba, sare nne na kupoteza
minne, huku Mnyama akiwa amecheza mechi 11 ya kushinda 9 na sare mbili wakiwa
haawajapoteza mchezo.
Kibarua kizito katika
mtanange huo kitakuwa kwa Kocha wa Mbao Salum Mayanga ukiwa mchezo wake wa
kwanza tangu achukue mikoba ya Ally Bushiri ‘Benitez’ baada ya kuvunjiwa
mkataba wake na Klabu hiyo kwa madai ya kutoridhishwa na matokeo waliyopata.
Mayanga anakuwa Kocha wa
tatu msimu huu kuinoa timu hiyo huku macho na masikio ya wengi yakimtazama jinsi
gani itaingia kuinusuru Mbao kushuka daraja msimu huu.
No comments:
Post a Comment