Rais
wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi na Ubunifu (TAFCA), Adrian Nyangamale
akishuhudia zana za jadi za wakazi wa Iramba na Mkalama.
NA MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO la Sanaa za
Ufundi na Ubunifu (TAFCA) limeeleza kwamba zana za jadi asili ya Wilaya za Mkalama
na Iramba ni sura ya jamii zetu kimatendo kwani zinabeba taswira ya maendeleo
kimaudhui.
Akizungumza leo katika
Tamasha la wenyeji wa wilaya za Mkalama na Iramba mkoani Singida (IDA)
lililofanyika kwenye hoteli ya African Heritage Beach Resort iliyoko Kigamboni
jijini Dar es Salaam, Rais wa Tafca, Adrian Nyangamale alisema tamasha hilo
linawagusa moja kwa moja na kueleza kwamba wataendelea kuwa sambamba na
waandaaji wa tamasha hilo ili kuendeleza sanaa hizo.
Nyangamale alisema
mojawapo ya mikakati itakayofanikisha Tafca kuwa karibu na IDA ni kupitia mradi
wa Utambuzi wa Wasanii Tanzania (TACIP) unaoendelea hapa nchini ambako hadi
sasa mikoa ya Mtwara, Dodoma, Pwani na Morogoro imeshapitiwa na mradi huo.
Alisema malengo ya
mradi huo ni kufika kila kona na Tanzania na kuwatambua wasanii wa sanaa za
ufundi na kuwataka Singida kujiandaa na mradi huo ili mkoa huo upate nafasi ya
kujitambulisha kwa serikali ambayo imeandaa mpango huo.
Aidha Nyangamale
alisema tamasha hilo ambalo ni la pili kufanyika anatamani lifanyike mkoani
Singida kwenye asili ya wakazi wa Mkalama na Iramba ili kuonesha uhalisia wa
tukio lenyewe ambalo litaleta mvuto zaidi kwa jamii.
Mkurugenzi wa Ukuzaji
Sanaa wa Baraza la Taifa la Sanaa (BASATA), Nsao Shalua alisema tamasha hilo ni
kwa ajili ya kuwarithisha vijana wa Singida, tamasha ambalo ni muhimu kwa
maendeleo ya sanaa.
Shalua ambaye pia ni
Mjumbe wa Tamasha la IDA alisema wazazi wanatakiwa kuwafundisha na kuwarithisha
watoto wao tamaduni za makabila yao na kutumia kauli ya baba wa Taifa, Mwalim
Julius Kambarage Nyerere aliyewahi kueleza kwamba Taifa lisilo na Utamaduni ni
sawa na Taifa mfu.
Mwenyekiti wa tamasha
hilo, Dk Alfred Mlima aliweka bayana malengo ya tamasha hilo ni kufahamiana
zaidi kwa wakazi wa wilaya hizo na kueleza kwamba tamasha hilo linatumika kama
sehemu ya furaha kwao.
“Watu wa jamii moja
wakikutana kuna elimu inapatikana kupitia mkutano huo, mtu hawezi kuendelea
kama hajui asili yake,” alisema Dk Mlima.
Dk Mlima alisema asilimia
kubwa ya Watanzania wanasahau asili yao, hata wao wanasahau hata tiba za
mitishamba ambayo ilikuwa ikiwasaidia na
kuhamia kwenye tiba za magharibi.
Naye Mwanamakati wa
tamasha hilo, Profesa Amos Majule wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
alisema jamii zetu hazitambui umuhimu wa maliasili zetu kama miti ya Miyombo ambazo
zinatakiwa kuenziwa na kutunzwa ili tuendelee kuwa nazo kwani umuhimu wake
katika jamii ni muhimu zaidi.
Profesa Majule alisema
kupitia tamasha hilo, jamii inatakiwa kuienzi miti ya asili, mali kale na
matukio mengine ya kihistoria ili vizazi vijavyo vipate kumbukumbu.
Mwenyekiti wa IDA,
Joseph Nsoza alisema lengo la umoja huo ni kukumbuka walipotoka kwani maisha
yamebadilika hasa ikizingatiwa vijana wengine wamekimbilia mijini na kusahau
walipotoka.
Nsoza alisema wameketi
na kugundua kwamba kuna mambo mengi ambayo ni ya asili yanayokosekana kwa
vijana wa sasa.
Katika tamasha hilo
kulikuwa na matukio mbalimbali kama maonesho ya zana za jadi za mkoa huo,
mnyimbo mbalimbali za asili ya makabila ya Wanyiramba na Waikizu, kukimbiza
kuku, mchezo wa soka na muziki wa dansi.
Awali kabla ya tamasha
hilo, umoja huo ulizindua Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) na viongozi hao
kutoa wito kwa wenyeji wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi katika umoja huo.
No comments:
Post a Comment