Msanii wa nyimbo za injili, Ester Tindos Kusekwa,
akitumbuiza wakati wa Sherehe ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, iliyofanyika Kisesa Mkoa wa Mwanza, hivi karibuni. (Picha na
Sitta Tumma).
NA SITTA TUMMA, MWANZA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalim, 'amemmwagia' pongezi msanii, Ester Tindos Kusekwa,
akisema kazi yake inafundisha mema Jamii.
Amesema msanii huyo wa jijini Mwanza, anayeimba nyimbo za
injili (Gospel) kazi yake imejaa ujumbe wa kuelimisha jamii, juu ya
matendo mema.
Waziri Ummy alitoa pongezi hizo kwa msanii huyo,
alipohutubia mamia ya wananchi mkoani Mwanza, katika Maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani, hivi karibuni.
Maadhimisho hayo ya 'Women's Day, ilifanyika kimkoa kwenye Uwanja wa Michezo, Kisesa Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.
"Nakupongeza sana mwimbaji, Ester Tindos Kusekwa. Umeimba vizuri, nimependa sana nyimbo zako.
"Nyimbo zako zimejaa ujumbe unaolenga kuleta maendeleo,
mshikamano na maendeleo ya nchi. Nasema hongera sana mwanamke
mwenzangu," alisema Waziri Ummy.
Katika Maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani, msanii
Ester anayetamba na Albamu ya Magufuli Jembe, alikuwa miongoni mwa
wasanii waliotumbuiza kwenye sherehe hizo.
Ester alipata kutuzwa vitu mbalimbali na viongozi wa kada
tofauti, waliohudhuria sherehe hizo, kulingana na kilichoonekana kukonga
nyoyo na nafsi zao.
"Mwakani nitakuwa Mkoa wa Simiyu, katika Siku ya Wanawake
Duniani. Nahitaji sana ushirikiano wa wasanii na jamii yote. Hongera
sana dada Ester Tindos Kusekwa," alisema waziri huyo.
Msanii Ester anayehitaji ushirikiano wa wadau, Serikali na
wasanii wenzake, kwa sasa anatamba na nyimbo mbalimbali, ikiwamo ya
Magufuli Jembe, inayobeba jina la albamu ya nyimbo sita.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Mwanza, Ester alisema
albamu nyingine iliyopo sokoni ni inayojulikana kwa jina la Nakalolela
ya mwaka 2010.
Alisema albamu hiyo iliyofanyiwa video mwaka 2015, ikiwa na
nyimbo saba za injili, inaelekeza namna jamii wanavyopaswa kuishi kwa
upendo, amani na kumcha Mungu.
"Ipo pia albamu ya Nyota Yangu. Hii nayo ina nyimbo saba ya mwaka 2018. Ni audio.
"Ile albamu ya Magufuli Jembe imebeba nyimbo za kijamii,
ukiwamo wimbo wa Tanzania ya viwanda, CCM juu, amani na wanawake,"
alisema Ester.
Ester alisema anahitaji sapoti kutoka kwa wadau wa muziki, ikiwamo Serikali na wasanii wenzake wa muziki.
No comments:
Post a Comment