HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 17, 2019

Al Bashir ahamishiwa gereza la Khartoum

 Aliyekuwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir.

KHARTOUM, SUDAN

RAIS wa zamani wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, aliyepinduliwa madarakani wiki iliyopita, amehamishiwa katika gereza la Kobar jijini Khartoum. 

Omar Hassan al-Bashiri anazuiliwa katika gereza la Kobar tangu Jumanne jioni wiki hii, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Kiongozi huyo wa zamani, ambaye alitawala Sudan tangu mwaka 1989, alikuwa mpaka sasa chini ya ulinzi wa kifungo cha nyumbani. 

Bashir, ambaye alielemewa na maandamano kwa miezi kadhaa, alishinikizwa kuachia ngazi na jeshi, Aprili 11 mwaka huu.

Jeshi kwa sasa ndilo linashikilia madaraka, licha ya shinikizo kutoka kwa waandamanaji na mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na nchi zeye nguvu duniani kutaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.

Mapema wiki hii Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, lilitaka jeshi nchini Sudan kukabidhi madaraka kwa raia kwa muda wa siku 15 zijazo, au nchi hiyo isimamishwe kuwa mwanachama wa Umoja huo.

Wito huu wa Umoja wa Afrika, umekuja wakati huu waandamanaji wakiendelea kusalia nje ya makao makuu ya jeshi kushinikiza serikali nchini humo kuundwa na raia wa kawaida.

Jumatatu wiki hii Luteni Jenerali Jalal al-Deen al-Sheikh, mmoja wa viongozi wa kijeshi alikutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia jijini Addis-Ababa na kusema kuwa, uongozi wa jeshi upo kwenye mchakato wa kumteua Waziri Mkuu, ambaye ataongoza serikali ya kiraia.

No comments:

Post a Comment

Pages