Mwenyekiti wa
Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dk. Faustine
Sambaiga (kushoto), akizungumza na wajumbe wa Bodi wakati wa kikao cha 40 cha
Bodi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kaimu Msajili wa Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali nchini, Neema Mwanga.
Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. John Jingu akizungumza na Mwenyekiti
Mpya wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dk.
Faustine Sambaiga (kulia) mara baada ya kikao cha 40 cha Bodi hiyo kilichofanyika
jijini Dodoma wa pili kushoto ni Kaimu Msajili wa Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali nchini, Neema Mwanga na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Usajili
Bw. Leornard Baraka. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW).
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kikao cha 40 wa Bodi
ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kimeyafutia usajili
Mashirika 6 Yasiyo ya Kiserikali kufanya kazi na kutoa huduma zake hapa nchini kufuatia kukiuka
Kanuni za Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lakini pia kufanya kazi
kinyume na Katiba zao kama zilivyowasilishwa kwa Msajili wa Mashirika hayo.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa Bodi ya Uratibu wa NGOs jijini Dodoma
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Neema Mwanga alisema kuwa uamuzi
huo umefikiwa baada ya ripoti ya uchunguzi wa Mashirika hayo
kuwasilishwa katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 17
Aprili, 2019.
Ameyataja Mashirika
yaliyofutwa kwa kutozingatia Sheria, Kanuni, taratibu na maadili ya nchini kuwa
ni Shirika la Community Health Education Services & Advocacy (CHESA), Kazi
Busara na Hekima (KBH Sisters), AHA
Development Organization Tanzania, Pathfinder Green City, Hope and Others na
HAMASA Poverty Reduction(HAPORE).
Aidha Bi. Mwanga alifafanua
kuwa Mashirika ya Community Health Education Services & Advocacy (CHESA), Kazi
Busara na Hekima (KBH Sisters), pamoja na
AHA Development Organisation Tanzania yamefutiwa
usajili kutokana na kosa la kukikuka Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
pamoja na Katiba iliyowasilishwa katika Ofisi ya Msajili kwa kuhamasisha
matendo yasiyofaa katika jamii mambo ambayo ni ukiukaji wa Sheria, maadili na
utamaduni wa Tanzania.
Aidha Bi. Mwanga
aliongeza kuwa Mashirika ya Pathfinder Green City, Hamasa
Poverty Reduction (HAPORE)
na Shirika la Hope and Others
yenyewe yaliomba kujitoa kwenye Orodha ya Msajili baada ya kutuhumiwa
kuendesha kazi zao kinyume na Katiba zake na hivyo Bodi ilielekeza
Mashirika hayo
kufutwa kwenye daftari la usajili.
Aidha, Msajili amefafanua
kuwa ufutwaji wa Mashirika hayo umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) (c)
cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005 inayosema
kuwa pale Msajili wa Mashirika hayo atakapopokea tuhuma kuhusu Shirika au Mashirika
yanayofanya kazi zake pasipo kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za nchini Msajili hupeleka notisi au onyo kwa Shirika
husika kujiteteta kabla ya kufikia maamuzi ya kufutiwa usajili.
Msajili ameongeza
kuwa endapo Ofisi ya Msajili isiporidhika na utetezi wa Shirika au Mashirika
yanayotuhumiwa kukiuka Sheria, Kanuni na taratibu itapeleka mashauri hayo
katika Kikao cha Bodi ya Uratibu wa Mashirika hayo na hao ndio wenye Mamlaka ya
kutoa idhini ya kufutwa au kutofutwa kwa Shirika.
Kwa upande wake Mwenyekiti
mpya wa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini Dkt. Faustine
Sambaiga amesema kuwa wameielekeza Sekretarieti kuyafutia usajili Mashirika
yote Yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa hayafuati Sheria, Kanuni na taratibu za
nchini ili kukidhi matakwa ya kisheria.
“ Kama Bodi tunamuagiza Msajili kuyafutia usajili Mashirika hayo kwani Bodi ndio yenye
Mamlaka ya kutoa idhini kwa Msajili wa
NGOs kuyafuta Mashirika au kutoyafuta” alisisitiza Dkt Sambaiga.
Mwenyekiti huyo wa
Bodi ameyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kufanya kazi kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za nchi na kuzingatia uwazi na
uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuchochea Ustawi na
Maendeleo ya Jamii.
Hatua hii ya
kuyafutia usajili Mashirika sita Yasiyo ya Kiserikali Nchini imekuja mara baada
ya kuundwa kwa Bodi ya Nne ya Uratibu wa Mashirika hayo chini ya uwenyekiti wa
Dkt. Faustine Sambaiga aliyeteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli hivi
karibuni kuongoza Bodi hiyo.
No comments:
Post a Comment