Jengo la Uatawla la hopitali ya Wilaya ya Kalambo ikiendelea kujengwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo (katikati), akitoa maagizo kwa timu ya
wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ikiongozwa na Mkurugenzi
mtendaji Msongela Palela (kulia) pamoja na kamati ya ulinzi na usalama
ya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Julieth Binyura (kushoto).
RUKWA, Tanzania
Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya
Wilaya ya Kalambo kusitisha mkataba na fundi anayehusika na ujenzi wa jengo la
maabara katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo huku akimtaka
Mkurugenzi huyo kutafuta chumba katika eneo hilo ili asimamie kwa karibu ujenzi
unaoendelea na kuhakikisha unaisha kwa wakati.
Ametoa
maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Suleiman Jafo hivi karibuni baada ya kuitaka
mikoa yote kusimamia ujenzi wa hospitali za wilaya na kufikia tarehe 13 hadi 25
Mei, 2019 majengo yote yawe yameshapauliwa na mikoa hiyo kutuma picha za
majengo saba ya hospitali hizo.
Kwa
kutekeleza hayo Mh. Wangabo amewaagiza mafundi wote wanaosimamia ujenzi wa
majengo hayo saba kuhakikisha wanafikia usawa wa linta ifikapo tarehe 10 mwezi
Mei mwaka huu na hatimae kumalizika kwa wakati.
Mh. Wangabo
ameyasema hayo alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kalambo
na kukutana na wataalamu wa halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo Msongela Palela pamoja na mafundi waliopewa mkataba kwaajili
ya ujenzi wa hospitali.
Baada ya
kutembelea alisema kuwa hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo ya
Wilaya ya Kalambo kwakua kasi ni ndogo pamoja na kujua kuwa kulikuwa na
changamoto nyingi hasa kipindi cha mvua ambapo barabara zilikuwa hazipitiki
hivyo vifaa mbalimbali kushindwa kufika kwenye eneo la ujenzi na kutahadharisha
kuwa sasa mvua zimeisha hivyo hakuna sababu ya kuendelea na kasi ile
iliyokuwepo.
“Lakini pia
nimegundua kuwa kuna wajenzi wengine hata ‘saiti’ hawapo na ujenzi wa majengo
yao unasuasua, sasa yule mjenzi wa maabara kule Mkurugenzi sitisha mkataba wake
mara moja na utafute mjenzi mwengine ambaye ataleta mafundi wengi na hili jambo
lichukue muda mfupi iwezekanavyo ili tarehe 10 mwezi Mei majengo yote haya saba
yawe yamefika kwenye hatua ya linta na sio vinginevyo,” alisisitiza.
Halikadhalika,
alisikiliza kilio cha vibarua wanaoendelea na ujenzi wa majengo ya hospitali
hiyo na kugundua kuwa kuna kusuasua kwa malipo ya vibarua hao na hivyo
kumuagiza Kamanda wa polisi wa Wilaya hiyo kuwakamata fundi anayehusika na
ujenzi wa jengo la utawala Fadhili Salum pamoja na msaidizi wake Amir Rajabu kwa kushindwa kuwalipa
vibarua wao tangu ujenzi huo uanze mwanzoni mwaka huu na kumtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo kufuatilia malipo ya vibarua hao kwa karibu ili wasiharibu
kazi.
Serikali imetoa
jumla ya Shilingi bilioni 105 kwa wilaya 67 kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi
wa hospitali za wilaya ambapo kila Wilaya ilipewa Shilingi bilioni 1.5 kwaajili
ya ujenzi wa majengo saba ya hospitali hizo ambapo mwisho wa ujenzi huo na majengo
hayo kuanza kutumika ni tarehe 30 June,
2019.
No comments:
Post a Comment