HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 18, 2019

Kangi Lugola: Watumishi Kitengo cha Malalamiko tekelezeni wajibu wenu


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola  na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, wakisikiliza maoni, hoja mbalimbali kwenye kikao kazi kilichoshirikisha watumishi wa Wizara hiyo kitengo cha kushughulikia malalamiko ya wananchi Kilicofanyika juzi Mjini Dodoma. (Picha na Veronica Mwafisi-MOHA) 
 
NA VERONICA MWAFISI, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa wito kwa watumishi wa Wizara hiyo kitengo cha kushughulikia malalamiko ya wananchi, kutekeleza wajibu wao wa kufuatilia na kuyapatia ufumbuzi wa haraka malalamiko wanayopokea.
Lugola aliyasema hayo jijini Dodoma juzi katika kikao kazi kilichoshirikisha watumishi wa kitengo hicho.
Aliwataka wafuatilie malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi ya taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
“Hakikisheni malalamiko mnayoletewa, mnayapatia ufumbuzi wa haraka bila kufika ngazi ya juu, tekelezeni wajibu wenu kwa ufanisi ili kujenga imani kwa wananchi (walalamikaji).
“Kama wananchi watajiridhisha kuwa kitengo hiki ni msaada mkubwa kwao, mtakuwa mmejijenga uaminifu na kuifanya Wizara ijitegemee kushughulikia malalamiko,” alisema.
Lugola alisisitiza umuhimu wa viongozi wanaoshughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi kuchukuliwa hatua kama itabainika wameshindwa kutimiza wajibu wao.
Alisisitiza umuhimu wa kubadili mfumo wa kushughulikia malalamiko akisema yanapofikishwa katika kitengo hicho yachunguzwe hapo hapo wizarani.
“Malalamiko yasirudishwe kwenye taasisi zinazolalamikiwa kama Polisi, Uhamiaji, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na NIDA…pia walalamikiwa waitwe na kuhojiwa.
“Lengo ni kupata suluhisho la malalamiko yanayotolewa ili kuleta uhuru, malalamiko yajibiwe kwa haraka na uwazikwa njia ya barua ama simu, malalamiko ambayo yataonekana hayana ukweli walalamikaji wapewe taarifa,” alisisitiza Lugola.
Aliongeza kuwa, malalamiko mengine hayapaswi kuchukua muda mrefu ili kutatuliwa akitolea mfano malalamiko ambayo aliyapokea kwa wananchi na kuyapatia ufumbuzi wa haraka kwenye ziara alizofanya katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, alitumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa kitengo hicho kwa kuyafuatilia malalamiko yanayotolewa na wananchi pamoja na kuyafanyia kazi kwa haraka.
Alisema kitendo cha kupokelewa, kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi ndani ya muda mchache, kitawezekana kama kila mtumishi anayeshughulikia malalamiko atawajibika ipasavyo ili kupunguza mrundikano wa malalamiko yanayotolewa.

Alitoa wito kwa watumishi wa kitengo hicho kwenda maeneo mbalimbali ambayo yana malalamiko ili kupata usahihi wa taarifa, kuzifanyia kazi na kutoa maamuzi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo na kutoka Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, NIDA na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

No comments:

Post a Comment

Pages