Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto), akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japani-JICA, Hiroshi Kato, walipokutana na kufanya mazungumzo kwenye Ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Washington DC-Marekani, kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la KImataifa-IMF. (Picha na Benny Mwaipaja, WFM-Washington DC).
Na Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C
Serikali
ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa-JICA inakusudia
kuipatia Tanzania mkopo nafuu pamoja na ruzuku wenye thamani ya zaidi ya dola milioni
345 za Marekani, sawa na takriban shilingi bilioni 794, kwa ajili ya kutekeleza
miradi mitatu ya maendeleo ikiwemo ukarabati wa barabara ya Arusha hadi Holili,
ukarabati wa Bandari ya Kigoma na Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira
Visiwani Zanzibar.
Ahadi
hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la JICA anayesimamia
Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw. Hiroshi Kato, alipokutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Mjini Washington
D.C nchini Marekani.
Ameitaja
miradi hiyo iliyoko mezani kwao inayosubiri kupatiwa fedha wakati wowote
kuanzia sasa kuwa ni mradi wa ukarabati wa barabara ya Arusha-Holili utakaopatiwa
mkopo wa dola milioni 221, Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira Zanzibar
utakaopatiwa fedha kupitia mkopo wa dola milioni 99 na mradi wa upanuzi wa Bandari
ya Kigoma ambao Japan itatoa ruzuku ya dola za Marekani milioni 25.
Bw.
Kato amesema kuwa Japan inajivunia ushrikiano wa muda mrefu kati yake na
Tanzania na kwamba iko tayari kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za
kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuitaka Serikali kuwasilisha miradi yake
ya kimkakati ambayo Japan itafadhili kupitia mikopo yenye riba nafuu pamoja na
ruzuku.
Akizungumza
na Mwakilishi huyo wa Japan katika Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Japan kwa uhusiano wake
mzuri na Tanzania na namna inavyo isaidia nchi kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo akitaja mmoja wa miradi hiyo kuwa ni barabara ya juu ya kwanza nchini
Tanzania katika makutano ya Tazara
Jijini Dar es Salaam, maarufu kama Daraja la Mfugale.
Dkt.
Mpango ameiomba Japan kupitia Shirika lake la JICA kutoa ruzuku na mikopo nafuu
ili kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha
kimataifa - SGR, Mradi wa kufua umeme wa Rufiji, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Msalato mkoani Dodoma, ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma, ujenzi wa
mtandao wa barabara, upanuzi wa bandari na miradi mingine ya kijamii.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango anaongoza ujumbe wa Tanzania katika
mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF,
inayofanyika mjini Washington DC nchini Marekani, ambapo ametumia fursa hiyo
kukutana na wadau wa maendeleo kupenyeza ajenda za maendeleo ya kiuchumi ya
Tanzania.
No comments:
Post a Comment