Na Jacquiline Mrisho
- MAELEZO
Mfuko mpya wa Hifadhi
ya Jamii wa PSSSF umekamilisha kulipa malimbikizo ya deni la wastaafu wapatao 9971
lililorithiwa kutoka katika mfuko wa PSPF.
Hayo yamesemwa leo
Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Sima alipokuwa akimuwakilisha Waziri mwenye
dhamana ya Mifuko ya Jamii kujibu swali la Mbunge wa Mbozi, Mhe. Paschal Haonga
lililohoji juu ya muda gani wastaafu katika Halmashauri za Wilaya nchini
watalipwa fedha zao.
Sima amesema kuwa
mfuko huo umekamilisha mfumo wa ulipaji mafao utakaowezesha kufanya malipo
katika ngazi ya Mkoa na hivyo kuwezesha mfuko kulipa mafao ndani ya muda
uliowekwa kisheria wa siku 60 tangu mwanachama anapowasilisha madai.
"Hadi kufikia
Februari 2019, mfuko wetu umetoa kiasi cha shilingi Bilioni 888.39 kwa ajili ya kuwalipa wastaafu waliotoka
katika mfuko wa PSPF", alisema Sima.
Akizungumzia kuhusu
tetesi za Serikali kutumia vibaya fedha za PSPF, Sima amesema kuwa mifuko hiyo
inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ambayo inasimamia muundo wa utawala na mfumo
wa maamuzi na usimamizi wa uwekezaji wa fedha za mfuko, hivyo, si kweli kwamba
Serikali inaweza kuingilia uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii au kufanya
maamuzi ya uwekezaji.
Aidha, Sima
amefafanua kuwa sheria za mifuko hiyo
chini ya Kanuni Namba 24 na 25 ya Kanuni mpya za Mafao ya Hifadhi ya
Jamii za Mwaka 2018 zimetoa wigo mpana zaidi kwa wanachama waliochangia kwa
miaka isiyopungua 10 kuweza kupata huduma hiyo tofauti na awali.
Naibu Waziri huyo aliongeza
kuwa mifuko hiyo inaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanachama
wake kupitia vikundi vya kuweka na kukopa katika maeneo ya kazi, mifuko hiyo
inaweza kutoa mikopo kwa SACCOs hadi asilimia 10 ya rasilimali za mfuko.
No comments:
Post a Comment