Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 17 Aprili 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha zote na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Dodoma
Katika mpango
kabambe wa Tanzania wa kufanya kilimo cha umwagiliaji kuwa kipaombele kikuu
yaani ASDP II kauli ya kuwa kilimo ni maji inajipambanua zaidi kwani
inazingatia matumizi bora ya ardhi na maji.
Katika kuongeza
ufanisi na tija katika kilimo kupitia umwagiliaji Serikali imejipanga vyema
kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mbinu bora za kilimo cha kisasa ikiwa ni
pamoja na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb)
ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 17 Aprili 2019 wakati akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe Rehema Juma Migila aliyetaka kufahamu Serikali
ina mpango gani wa kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji katika Manispaa ya Tabora,
kwa kutumia maji kutoka Bwawa la Igombe baada ya ujio wa maji kutoka Ziwa
Victoria kufika Tabora.
Mhe Mgumba alisema kuwa wakati wa kupanga matumizi ya maji kutoka katika chanzo, utunzaji
wa mazingira na matumizi ya jamii hupewa umuhimu zaidi kabla ya matumizi
mengine.
Ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji kutoka
Ziwa Victoria umelenga zaidi katika kupunguza upungufu wa maji uliopo kwenye
Manispaa ya Tabora ambayo kwa sasa inahudumiwa na Bwawa la Igombe. Maji hayo ni
kwa ajili ya matumizi ya kijamii tu kwani hayatatosha kwa kilimo cha
umwagiliaji.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa kuongeza
uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa tija na kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi, Wizara ya kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ina Mpango
Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji unaotekelezwa kuanzia 2018/2019 hadi 2035/2036
ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo katika Manispaa ya Tabora, mpango huo
umejumuisha uboreshaji na ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Imalamihayo, Inala,
Magoweko na Bonde la Kakulungu.
Aliongeza kuwa
rasilimali maji ni muhimu katika jamii na kama itawekwa vizuri matumizi yake
katika kila hatua huleta manufaa makubwa kwa kilimo kupitia
umwagiliaji na kupata nishati ya umeme kwenye maporomoko.
No comments:
Post a Comment