Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria
imejipanga kuimarisha mfumo madhubuti wa kikatiba na kisheria ili kufanikisha
utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria,
Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa akiwasilisha Bungeni Mpango na
Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Balozi Mahiga amesema kuwa katika mwaka huu wa
fedha, wizara hiyo itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria kwa
Umma ambapo imeainisha maeneo mahususi
ya vipaumbele na kuyawekea mikakati ya utekelezaji.
"Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele
hivyo vitakavyoisaidia nchi kusonga mbele, katika Bajeti ya Mwaka 2019/20
Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 55,175,163,302 kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo", alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga amevitaja baadhi ya vipaumbele
vya Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo vikiwemo vya kukamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya
Sheria kwa ajili ya mambo ya kisheria na utekelezaji wake kuwa; kufuatilia na
kutathmini utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maboresho katika
mfumo wa utoaji haki nchini pamoja na kushiriki katika masuala mbalimbali ya
kikanda na kimataifa yanayoihusu wizara.
Vile vile kwa upande wa Mahakama ya Tanzania.
baadhi ya vipaumbele ni kuanza ujenzi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania jijini Dodoma pamoja na kuendelea na ujenzi wa Mahakama nchini kote
zikiwemo Mahakama Kuu mbili zinazoendelea kujengwa mkoani Kigoma na Mara; na
kuanza kujenga nyingine katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Dodoma na Singida.
Aidha,
Balozi Mahiga ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na
utekelezaji wa vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 vikiwemo
vya wananchi kuwa na uhakika kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu za kimahakama,,
kupatikana kwa ofisi za kudumu za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa huduma za kisheria kupitia
TEHAMA pamoja na kupatikana kwa kiasi
kikubwa cha fedha na mali nyingi kilichookolewa na kurejeshwa Serikalini.
No comments:
Post a Comment