Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali imepanga kufanya
mabadiliko ya kanuni za matumizi ya nyavu upande wa bahari ili wavuvi waweze
kutumia nyavu za milimita nane badala ya milimita kumi zilizokuwa zikitumika
awali.
Hayo yamesemwa leo, Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi lililohoji kuwa ni lini Serikali
itakuwa tayari kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Victoria kama inavyofanya upande
wa Bahari ili kuweza kuruhusu matumizi ya nyavu za chini ya milimita nane.
Ulega amesema kuwa kwa mujibu wa
Sheria, nyavu za kuvulia dagaa zenye ukubwa wa macho chini ya milimita nane
zimekatazwa kutumika kwa uvuvi wa dagaa katika maji baridi ikiwemo maeneo ya
maziwa kwa sababu tafiti zinaonyesha kuwa aina hiyo ya nyavu ikitumika itavua
dagaa wachanga hivyo kuathiri uvuvi wa dagaa.
"Taasisi
ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania itafanya utafiti na endapo itaridhika itaruhusu
wavuvi wanaovua ziwani wavue kwa kutumia aina hiyo ya nyavu, kwa upande wa
bahari Serikali imeielekeza TAFIRI
kufanya utafiti na kujiridhisha kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kanuni kwa
haraka ili ikiwezekana tuweze kutumia nyavu za milimita nane zitakazoweza kuwanufaisha wavuvi wa upande wa bahari",
alisema Ulega.
Amefafanua
kuwa kwa upande wa bahari, nyavu zilizokuwa zikitumika kuvua dagaa ni milimita
kumi lakini maoni ya wadau wengi yanaonesha kuwa milimita kumi zimeshindwa
kuvua dagaa ndio maana Serikali imeamua kufanya utafiti huo ili kuona kama
inawezekana wavuvi wa bahari kutumia nyavu za milimita nane.
Akizungumzia
kuhusu uvuvi wa samaki aina ya Gogogo, Ngele na Mingu waliopo katika Ziwa
Victoria, Naibu Waziri Ulega amesema kuwa katika mabadiliko ya Kanuni
yanayofanyika hivi sasa Serikali imezingatia kufanya makubaliano ya kupitisha
kanuni rasmi itakayoruhusu uvuaji na matumizi ya aina hizo za samaki.
Waziri Ulega
ametoa rai kwa wavuvi kuendelea kuzingatia sheria na kanuni zilizopo kwani Sheria
na kanuni hizo zinalenga uvuvi unaofanyika nchi uwe endelevu na wenye tija.
No comments:
Post a Comment